News

TANROADS YATOA TAHADHARI YA MVUA ZA EL NIÑO, VIFAA VYA MWITIKIO VYATAYARISHWA

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, ametoa tahadhari kwa wananchi na watumiaji wa barabara kuchukua hatua za usalama wakati wa kipindi cha mvua zinazotarajiwa kutokana na hali ya El Niño, huku akieleza kuwa TANROADS imejiandaa kwa kuweka tayari vifaa na mifumo ya mwitikio kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Mhandisi Besta ametoa tahadhari hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, akieleza kuwa TANROADS inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kujiandaa na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo kufanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara na kuhakikisha maeneo hatarishi yanafanyiwa matengenezo kwa wakati.

Amesema kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuna uwezekano wa kujitokeza kwa hali ya El Niño katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026, ambapo baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

“Tunachukua hatua za kuhakikisha vifaa na mifumo yetu ya mwitikio inakuwa tayari, ili pale changamoto zinapojitokeza tuweze kuchukua hatua kwa wakati,” amesema Mhandisi Besta.

Ameeleza kuwa TANROADS imeelekeza mikoa yote kufanya ukaguzi wa barabara, madaraja, makaravati, mitaro na maeneo mengine yanayoweza kuwa hatarishi wakati wa mvua, pamoja na kusafisha mifumo ya kupitisha maji na kushughulikia maeneo yenye udhaifu kabla ya mvua kuanza kwa nguvu.

Aidha, amesema TANROADS inaendelea kuimarisha matengenezo kinga katika maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa mara kwa mara na mafuriko, huku ikiendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na utoaji wa taarifa kwa kushirikiana na TMA pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na usimamizi wa maafa.

Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, katika kipindi hicho TANROADS itaendelea kuwa tayari kuratibu mwitikio wa haraka kwa kupeleka wataalamu, vifaa na wakandarasi katika maeneo yatakayoathirika, kwa lengo la kurejesha huduma za miundombinu ya barabara kwa wakati.

Ametoa wito kwa wananchi na watumiaji wa barabara kutoa taarifa mapema wanapoona uharibifu wa miundombinu ya barabara au hali yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji.

Mhandisi Besta pia amewataka wananchi kuwa makini na kuepuka kuvuka maeneo yaliyojaa maji, mito au madaraja yenye maji mengi bila kuwa na uhakika wa usalama wa eneo hilo.

“Ni vyema kuchukua tahadhari hata kama itabidi kuchelewa safari kwa muda kidogo ili uwe na uhakika wa kusafiri kwa usalama. Tukumbuke msemo maarufu wa Kiswahili usemao, KAWIA UFIKE,” amesema.

Amesisitiza kuwa usalama wa wananchi unapaswa kupewa kipaumbele wakati wote wa kipindi cha mvua, huku akieleza kuwa TANROADS itaendelea kufuatilia hali ya miundombinu ya barabara nchini na kuchukua hatua za haraka pale changamoto zitakapotokea.