News

TANROADS YATOA WITO KWA WATANZANIA KUTUMIA FURSA ZA UWANJA WA NDEGE WA MSALATO

Dodoma

 Ujenzi wa miundombinu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2026, huku ujenzi wa majengo ukitarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Desemba 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema Wakala inaendelea kufuatilia kwa karibu programu za kazi, upatikanaji na ufungaji wa vifaa, uratibu wa wakandarasi, utekelezaji wa kazi zinazotegemeana, pamoja na kukamilishwa kwa taratibu za kimkataba.

Mhandisi Besta amesema mradi huo umetoa jumla ya ajira 9,059 kwa Watanzania katika kipindi chote cha utekelezaji, ambapo sehemu ya kwanza imetoa ajira 3,571 na sehemu ya pili ajira 5,488. Aidha, jumla ya wafanyakazi wa kigeni 47 wameshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.

Ametoa wito kwa Watanzania, hususan wakazi wa Dodoma, kutumia fursa zitakazotokana na uwepo wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kukuza biashara zao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amesema uwanja huo utatoa fursa kwa biashara zinazohitaji usafirishaji wa haraka wa bidhaa, zikiwemo bidhaa za kilimo kama matunda na mboga mboga, samaki, kuku na maua. Aidha, amesema uwepo wa uwanja huo utatoa nafasi ya kukuza sekta ya utalii nchini.