Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imewataka wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Nne (BRT 4) kuendelea na ujenzi huku wakichukua hatua za kuzuia athari za mvua kubwa za El Niño.
Meneja wa Mradi wa BRT 4, Mhandisi Allen Natai, amesema wakandarasi wanapaswa kuhakikisha vifusi vya ujenzi havizuii mitaro na njia za maji, pamoja na kuhakikisha maeneo hayo yanasafishwa ili kuwezesha mtiririko mzuri wa maji wakati wa mvua.
Ametaja maeneo ya ITV, Best Bite na Boko Bashihaya kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji uangalizi maalum, huku akimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa Daraja la Salender.
Amesema daraja jipya linatarajiwa kujengwa katika eneo la daraja la zamani la Salender, wakati madaraja yanayotumika kwa sasa yatafanyiwa ukarabati ili kuimarisha usalama nauimara wa miundombinu.
Hatua hizo zinalenga kuhakikisha ujenzi wa BRT 4 unaendelea kwa usalama, huku miundombinu ya kupitisha maji ikifanya kazi ipasavyo katika kipindi cha mvua kubwa.