News

TANROADS YAONGEZA UFUATILIAJI WA HALI YA BARABARA KABLA YA MVUA ZA EL-NINO.

Morogoro

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro imeongeza ufuatiliaji wa hali ya barabara na madaraja katika mkoa huo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua za El-Nino.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Baraka Mwambage, amesema wataalamu wa Wakala hiyo wamefanya tathmini ya mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 2,071 pamoja na madaraja 1,032, ili kubaini maeneo yanayohitaji uangalizi wa karibu wakati wa msimu wa mvua.

Amesema tathmini hiyo imewezesha TANROADS kutambua maeneo 49 yanayohitaji ufuatiliaji maalumu na hivyo kuweka mkazo wa maandalizi kulingana na hali ya maeneo hayo.

“Baada ya Serikali kutoa tahadhari ya El-Nino, tulifanya tathmini katika mtandao wetu wote na kubaini maeneo yanayohitaji uangalizi maalumu. Hatua hii inatusaidia kuelekeza ufuatiliaji na maandalizi yetu kwa wakati,” amesema Mwambage.

Amesema TANROADS itaendelea kufuatilia hali ya barabara, madaraja na makalavati na kuchukua hatua za tahadhari pale inapohitajika, huku wananchi wakitakiwa kutoa taarifa mapema endapo wataona changamoto katika miundombinu ya barabara.