Kilimanjaro
Ofisi ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro inaendelea na ukaguzi na matengenezo ya madaraja, makalvati na mifereji ya maji katika barabara Kuu na za Mikoa, ikiwa ni hatua za kujiandaa na mvua kubwa zinazotarajiwa.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando, amesema baada ya ukaguzi wa miundombinu hiyo, wameanza kurekebisha maeneo yaliyobainika kuwa na hitilafu, ikiwemo kusafisha madaraja na kuondoa michanga, miti na uchafu unaozuia mtiririko wa maji.
Amesema pia wanaendelea na ukarabati wa Daraja la Makanya lililopo katika barabara ya KIA JCT – Moshi – Himo – Same– Mkomazi, ikiwemo kuandaa eneo kwa ajili ya kuweka mawe makubwa (boulders) na zege ili kuimarisha mkondo wa maji na miundombinu ya barabara.
Aidha, TANROADS inaendelea kuzibua mikondo ya maji na kuchimba makinga maji katika maeneo mbalimbali kama sehemu ya maandalizi ya mvua za El Niño.
Mhandisi Kyando amewataka wananchi kutozoea kutupa taka kwenye mifereji, makalvati na madaraja, kwa kuwa uchafu huo unaweza kuziba njia za maji na kusababisha mafuriko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, ameipongeza TANROADS kwa hatua hizo na kusisitiza kazi za matengenezo zifanyike kwa ubora na zikamilike kwa wakati kabla ya kuanza kwa mvua hizo.
Hivi karibuni, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri uwepo wa mvua kubwa zinazoweza kuwa juu ya wastani katika maeneo mbalimbali nchini.