Ofisi ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga inaendelea kuchukua hatua za maandalizi na tahadhari kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino zinazotarajiwa kunyesha baadaye mwezi Oktoba, kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesye, amesema kuwa TANROADS inaendelea na maandalizi kwa kushirikiana na wakandarasi, ikiwemo kuondoa mchanga na uchafu kwenye madaraja, makalavati na mifereji iliyopo kwenye barabara kuu na barabara za mikoa, ili kuhakikisha njia za kupitisha maji zinaendelea kuwa wazi wakati wa mvua.
Amesema sambamba na maandalizi hayo, TANROADS inaendelea kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuhusu athari ambazo mvua kubwa zinaweza kusababisha kwenye miundombinu ya barabara, pamoja na hatua wanazopaswa kuchukua ili kujilinda wao na mali zao.
Mhandisi Ntuli amewataka wananchi kuacha kuchimba mchanga chini au karibu na madaraja, pamoja na kutupa taka kwenye mifereji, makalavati na madaraja, kwa kuwa vitendo hivyo vinaweza kuathiri uimara na uwezo wa miundombinu hiyo kupitisha maji, na hivyo kuongeza hatari ya mafuriko na uharibifu wa barabara.
Amesema elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa wananchi na watumiaji wa barabara ili kuongeza uelewa kuhusu namna ya kutumia na kutunza miundombinu ya barabara wakati wa msimu wa mvua.
Mhandisi Ntuli amesema Mkoa wa Shinyanga una jumla ya madaraja 114 ya aina mbalimbali, yakiwemo madaraja makubwa ya Ubagwe II na Kasenga yaliyopo kwenye barabara ya Mwabomba–Igombe River, pamoja na Daraja la Ng’hwande lililopo kwenye barab0ara ya Nyandekwa – Ng’hwande. Madaraja hayo yote yapo katika Wilaya ya Kahama.
Amesema TANROADS itaendelea kufuatilia hali ya miundombinu ya barabara na kuchukua hatua stahiki kulingana na hali itakavyojitokeza wakati wa msimu wa mvua, huku wananchi wakihimizwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika.
Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa angalizo kupitia utabiri unaoonesha uwezekano wa kuwepo kwa mvua zaidi ya kiwango cha wastani, ambazo zinaweza kusababisha madhara kwa wananchi na mali zao, pamoja na uharibifu wa miundombinu mbalimbali.