Kigoma.
Agizo la Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, la kutaka vijana wazawa wapewe kipaumbele katika kupata ajira kwenye miradi ya ujenzi limeanza kuzaa matunda baada ya vijana 12 kuajiriwa katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha Manyovu, mkoani Kigoma.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Elsony Mweladzi, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, ambao kwa sasa umefikia asilimia 35 ya utekelezaji.
Mhandisi Mweladzi amesema ziara hiyo imelenga kujiridhisha na utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, hususan kuhusu mkandarasi kutoa fursa za ajira kwa vijana wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mradi.
Amesema kuwa katika utekelezaji wa agizo hilo, kijana mmoja aliyewasilisha ombi la kuomba ajira wakati wa ziara ya Waziri amepewa fursa hiyo, sambamba na vijana wengine 12, baada ya kushiriki katika mchakato wa usaili na kipindi cha uangalizi.
“Moja ya maelekezo ya Mheshimiwa Waziri ni kutoa fursa za ajira kwa wakazi wa eneo hili. Tumekuja kujiridhisha kama maelekezo hayo yametekelezwa na tumegundua kuwa mkandarasi ameyatekeleza,” amesema Mhandisi Mweladzi.
Mhandisi Mweladzi amempongeza mkandarasi kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali na kuwapa vijana wazawa fursa ya kushiriki katika mradi huo, huku akiwapongeza vijana hao kwa kufanikiwa kupita katika usaili na kipindi cha uangalizi na hatimaye kupata mikataba rasmi ya ajira.
Ameongeza kwa kusema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wananchi wanaozunguka miradi ya maendeleo wanapata manufaa ya moja kwa moja kupitia fursa zinazozalishwa na miradi hiyo.
Kwa upande wake, mmoja wa vijana walioajiriwa katika mradi huo, Amoni Kanyabarai, amesema ujio wa Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, katika eneo hilo uliwafungulia fursa ya kupata ajira.
Amesema baada ya kuwasilisha ombi la ajira, yeye pamoja na vijana wengine walipata nafasi ya kushiriki katika mchakato wa usaili na kipindi cha uangalizi, hatua iliyowawezesha kufikia hatua ya kusaini mikataba rasmi ya ajira.
“Ujio wa Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega umefungua fursa ya sisi vijana kupata ajira. Tumeomba kazi, tumepitia usaili na kipindi cha uangalizi, na sasa tumefanikiwa kusaini mikataba kwa ajili ya kufanya kazi katika ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha Manyovu,” amesema Kanyabarai.
Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha Manyovu unaendelea kutekelezwa kwa hatua mbalimbali, ambapo hadi sasa umefikia asilimia 35 ya utekelezaji.
TANROADS Mkoa wa Kigoma imeeleza kuwa itaendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali, huku ikihakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyokusudiwa na kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na uwepo wa miradi katika maeneo yao.