News

TANROADS MBEYA YAONGEZA KASI UJENZI WA NJIA NNE BARABARA YA TANZAM

Mbeya.

Ujenzi wa mradi wa upanuzi wa Barabara ya TANZAM kuwa na njia nne katika Mkoa wa Mbeya umefikia asilimia 45, huku Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya ukisisitiza kuongezwa kwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali katika kuboresha miundombinu nchini.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema Mbeya ni miongoni mwa mikoa yenye miradi mikubwa ya kimkakati, na kwamba mradi wa ujenzi wa njia nne katika Barabara ya TANZAM ni miongoni mwa miradi hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa wananchi na uchumi wa Taifa.

Mhandisi Bishanga amesema Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa  imeelekeza mradi huo kutekelezwa kwa kasi, huku TANROADS ikiendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa kazi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa ufanisi na kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.

Amesema maelekezo ya Serikali, pamoja na usimamizi wa Mkoa wa Mbeya, yanalenga kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa ubora huku haki, usalama na maslahi ya wananchi wanaotumia barabara hiyo yakipewa

Ameongeza kwa kusema TANROADS tayari imeanza kutekeleza maagizo ya Serikali Kupitia mkuu wa Mkoa imemuelekeza mkandarasi kuanza kuweka lami katika maeneo yenye uhitaji mkubwa, ikiwemo eneo la Mama John, Ilomba na Nanenane, ambayo tayari yameingizwa katika mpango kazi wa utekelezaji wa mradi.

Aidha, amesema mkandarasi ameelekezwa kuanza mapema kazi za ujenzi wa mitaro pamoja na ukataji wa baadhi ya maeneo ya milima, hususani katika maeneo ambayo yanaweza kuathiriwa na mvua, ili kupunguza changamoto kwa wananchi na kuhakikisha maji yanapita vizuri bila shida yeyote.

Mha.Bishanga amesema Barabara hiyo pia inaunganisha shughuli za usafirishaji na biashara kuelekea Bandari ya Dar es Salaam, hivyo upanuzi wake kuwa na njia nne unatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji, kupunguza msongamano na kuimarisha biashara katika ukanda huo.

TANROADS Mkoa wa Mbeya imeendelea kusisitiza kuwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo itaenda sambamba na kuhakikisha viwango vya ubora vinafuatwa, usalama wa watumiaji wa barabara unalindwa na wananchi wanaendelea kupata manufaa ya mradi katika kipindi chote cha ujenzi.