News

TANROADS SONGWE YAJIANDAA NA VIFAA VYA DHARURA KUKABILI MVUA ZA EL NINO

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe umejiwekea utayari wa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2026, ikiwa ni pamoja na kuandaa vifaa vya dharura kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya barabara endapo itaharibiwa na mvua hizo.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Fredrick Mande, amesema Wakala umeendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa pamoja na miongozo inayotolewa na mamlaka husika, hatua iliyowezesha kuanza maandalizi mapema.

Amesema TANROADS Songwe imefanya ukaguzi wa mtandao wa barabara unaosimamiwa na Wakala katika Mkoa huo wenye jumla ya takribani kilomita 1,035, ikiwemo barabara za mkoa na barabara kuu, kwa lengo la kubaini maeneo hatarishi na kuchukua hatua za kinga kabla ya mvua kuanza.

Katika hatua muhimu ya maandalizi, Mhandisi Mande amesema tayari TANROADS Songwe imefanya maandalizi ya makalvati ya chuma kwa ajili ya matumizi ya dharura, ambayo yanaweza kusaidia kurejesha miundombinu ya barabara kwa muda mfupi pale itakapoharibiwa na maji.

Aidha, amesema Wakala umeendelea na mchakato wa upatikanaji wa makalvati ya plastiki, ambayo yanaweza kutumika kwa urahisi na kwa haraka katika kurejesha maeneo ya barabara yatakayokatika au kuathiriwa na maji.

Mhandisi Mande amesema maandalizi hayo pia yanahusisha ushirikiano na wakandarasi wanaotekeleza kazi za barabara mkoani Songwe, ambapo wamepewa maelekezo ya kuhakikisha miundombinu muhimu ikiwemo mitaro, madaraja na makalvati inakuwa katika hali nzuri kabla ya mvua kuanza.

Amesema wakandarasi wameelekezwa pia kuhakikisha vifaa na mitambo yao inakuwa tayari ili kuruhusu hatua za haraka kuchukuliwa endapo kutatokea uharibifu wa barabara au miundombinu yake.

Ameongea kwa kusema kuwa  maeneo yote yaliyobainika kuwa hatarishi tayari yameainishwa na Wakala, hivyo hatua za maandalizi zinaendelea kwa kushirikiana na wakandarasi ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua.

TANROADS Songwe imesisitiza kuwa uwepo wa vifaa vya dharura pamoja na maandalizi ya mapema ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa endapo miundombinu ya barabara itaathiriwa na mvua za El Niño, marekebisho yanafanyika kwa wakati na barabara zinaendelea kupitika.

Maandalizi hayo yanaendelea huku TANROADS Songwe ikiendelea kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa na kufanya tathmini ya maeneo hatarishi, kwa lengo la kulinda miundombinu ya barabara na kuhakikisha usalama na mwendelezo wa usafiri kwa wananchi wakati wa msimu wa mvua.