Shinyanga
Wananchi wa Kijiji cha Lunguya wameahidi kulinda miundombinu ya Barabara ya Kahama–Bulyanhulu–Kakola baada ya kukamilika kwa ujenzi, ikiwemo taa za barabarani, ili isiharibiwe au kuibiwa.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Bw. Paschal Joachim, amesema taa hizo zitaongeza usalama kwa wapita njia na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli mbalimbali nyakati za usiku.
Ameishauri TANROADS Shinyanga kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi na utunzaji wa miundombinu hiyo.
Ameishukuru Serikali kwa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, akisema ilikuwa kilio cha muda mrefu cha wananchi, na kuomba maeneo ambayo bado hayajafikiwa na barabara za lami nayo yapewe kipaumbele.
Amesema hakuna mgogoro wa fidia, kwani wananchi wote waliopitiwa na mradi wamelipwa kwa wakati. Aidha, wananchi wengi wamepata ajira katika mradi huo na kujifunza ujuzi utakaowawezesha kujiajiri baada ya mradi kukamilika.
Mmoja wa wanufaika, Dancan Matumla, anayefanya kazi chini ya mkandarasi CCECC, amesema ajira hiyo imemsaidia baada ya kukaa bila kazi kwa muda mrefu na kumpatia ujuzi wa kujiendeleza.
Kwa upande wake, Michael Yohana, mwendesha bodaboda na mkazi wa Segese, amesema barabara hiyo ya lami itaongeza kipato kwa kuwa wataweza kubeba abiria mara nyingi zaidi ikilinganishwa na kipindi ambacho barabara ilikuwa ya vumbi.