News

TANROADS YAENDELEA NA MATENGENEZO YA BARABARA YA GEHANDU–BABATI

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara unaendelea na kazi za uboreshaji wa miundombinu ya barabara mkoani humo, ikiwemo matengenezo ya barabara ya Gehandu–Babati.

Matengenezo hayo yanahusisha maeneo korofi katika barabara hiyo, ambapo awamu ya kwanza inahusisha uboreshaji wa sehemu yenye urefu wa kilomita 15 kuanzia mpakani mwa Mkoa wa Manyara na Singida.

Hadi sasa kilomita 10 kati ya hizo 15 zimekamilika na barabara hiyo imeanza kupitika vizuri katika sehemu zilizofanyiwa matengenezo.

Aidha, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara, Mhandisi Dutu Masele, amesema kuwa kuna mpango wa kufanya matengenezo mengine yatakayohusisha kilomita 20 kuelekea Katesh mjini.

Mhandisi Masele ameongeza kwa kusema kuwa, kukamilika kwa matengenezo hayo kutasaidia kuboresha hali ya barabara na kurahisisha usafiri kwa wananchi na watumiaji wengine wa barabara hiyo.

“Matengenezo hayo yatasaidia barabara kupitika vizuri baada ya kilomita 20 kukamilika hadi Katesh,” alisema Mhandisi Masele.

Uboreshaji wa barabara hiyo unatarajiwa kuimarisha usafiri na usafirishaji katika maeneo yanayounganishwa na barabara ya Gehandu–Babati, pamoja na kuongeza urahisi wa wananchi na wafanyabiashara kutumia njia hiyo.