News

DARAJA LA KALEBE KUIMARISHA USAFIRISHAJI NA SHUGHULI ZA KIUCHUMI KAGERA

Ujenzi wa Daraja la Kalebe mkoani Kagera unatarajiwa kuimarisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kuimarisha muunganiko wa maeneo mbalimbali kupitia mtandao wa barabara nchini.

Daraja hilo lenye urefu wa mita 60 na upana wa mita 11 limejengwa kwa viwango vya kisasa, likiwa na uwezo mkubwa zaidi wa kubeba mizigo ikilinganishwa na daraja la awali lililokuwa na uwezo wa tani 10.

Msimamizi wa ujenzi, Mhandisi Kenneth Mkude, amesema mradi huo pia umehusisha kuinua tuta la barabara pamoja na maungio yake kwa urefu wa kilomita 1.5, hatua inayolenga kupunguza athari za mafuriko na kuhakikisha barabara inapitika kwa usalama wakati wa mvua.

“Daraja hili ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha miundombinu ya barabara, kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa, na kuwezesha shughuli za kiuchumi kuendelea bila vikwazo,” amesema.

Ametoa wito kwa watumiaji kutunza miundombinu hiyo na waenda kwa miguu kutumia njia maalum zilizotengwa kwa ajili yao ili kuimarisha usalama.

Ujenzi wa daraja hilo unaotekelezwa na kampuni ya wazawa ya Mirembe Construction Co. Ltd umefikia asilimia 95. Mkandarasi amekamilisha sehemu ya kupita magari na anaendelea na kazi za usafishaji, ikiwemo kuondoa udongo na vifusi chini ya daraja ili kuwezesha maji kupita kwa urahisi.