News

BARABARA KIBADA–KIMBIJI KUCHOCHEA USAFIRISHAJI WA BIDHAA KUTOKA ENEO MAALUM LA VIWANDA

Barabara ya Kibada–Masonga Junction–Kijaka–Chemeni/Kimbiji yenye urefu wa kilomita 41, Wilaya ya Kigamboni, inatajwa kuwa kiungo muhimu cha kuchochea shughuli za uzalishaji na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka eneo hilo maalum la viwanda jijini Dar es Salaam kwenda mikoa mbalimbali nchini na nchi jirani.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema barabara hiyo ni ya kimkakati kutokana na kupita katika maeneo yenye viwanda mbalimbali, ikiwemo kiwanda cha saruji cha Kimbiji, viwanda vya maji na vigae.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa Kigamboni, huku pia ikifungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi na wafanyabiashara wanaotegemea miundombinu hiyo.

Kwa sasa, Kyamba amesema utekelezaji wa mradi huo kilomita 13 zimekamilika kwa kuwekwa lami na alama za barabarani.maeneo yaliyosalia yanaendelea kujengwa katika hatua mbalimbali, ikiwemo uwekaji wa tabaka la msingi (Base Course), C1 na G15, huku madaraja mawili makubwa yaliyopo kwenye njia hiyo tayari yakiwa yamekamilika.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya wazawa, Estim Company Limited, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Kigamboni.

Aidha, Kyamba amewataka wananchi kushirikiana katika kulinda samani, alama na miundombinu ya barabara hiyo ili iweze kudumu na kutoa huduma iliyokusudiwa.

Katika hatua nyingine, ametoa pia wito wa kuzingatia usalama barabarani, akisema kasi ya magari imeongezeka katika maeneo yaliyowekwa lami, hivyo wananchi wanapaswa kuwa waangalifu wanapovuka barabara.