News

TANROADS KIGOMA YAJIPANGA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MVUA ZA EL-NINO

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma umejipanga kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino, ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Elsony Mweladzi, amesema kuwa Wakala tayari umeanza kuchukua hatua za tahadhari kwa kushirikiana na wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya barabara mkoani humo.

Amesema TANROADS imefanya mawasiliano na wakandarasi  ili kuhakikisha wanakuwa tayari kutoa huduma za dharura endapo mvua hizo zitasababisha changamoto katika miundombinu ya barabara, ikiwemo kuziba kwa makaravati, kuharibika kwa barabara, kujaa kwa maji pamoja na changamoto nyingine zinazoweza kujitokeza.

Aidha, Mhandisi Mweladzi amewataka wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuwa sehemu ya juhudi za kulinda miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha hawafanyi shughuli zinazoweza kusababisha uharibifu wa barabara, makaravati na mifumo ya kupitisha maji.