News

KIGOMA YAZIDI KUPENDEZA, TANROADS YAWEKA MIUNDOMBINU YA KISASA KURAHISISHA USAFIRI

KIGOMA, 2 Septemba 2026.

Mkoa wa Kigoma unazidi kubadilika na kupendeza kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara inayolenga kurahisisha usafiri, kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara pamoja na kuboresha mandhari ya mji.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Elsony Mweladzi, amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 mkoa umeendelea kuweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya barabara kwa kuweka njia za kisasa za kugeuzia magari, taa za kisasa, vituo vya kusubiria mabus ya abiria (bus shelter) pamoja na mabango makubwa ya matangazo.

Amesema njia hizo za kugeuzia magari zimewekwa katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kurahisisha usafiri kwa wananchi wanaokwenda katika maeneo muhimu ya mji, ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Soko la Mwembe Togwa na Mwanga, ambapo wananchi sasa wanaweza kugeuza magari kwa urahisi bila kulazimika kwenda umbali mrefu hadi SIDO kama ilivyokuwa awali.

Mhandisi Mweladzi amesema pia TANROADS imeweka taa za kisasa katika eneo la Mnarani, jirani na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, hatua ambayo siyo tu imeongeza mwonekano na uzuri wa mji, bali pia imeongeza usalama kwa watumiaji wa barabara nyakati za usiku.

Aidha, amesema Mkoa wa Kigoma unatarajia kuwa na vituo vya kusubiria mabasi vya abiria (bus shelter) vitakavyojengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa vinavyoonekana katika baadhi ya nchi duniani, ikiwemo China na Dubai. Amesema maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo yanaendelea na mkandarasi tayari ameshapatikana, hivyo wananchi wanatarajia kuona mabadiliko katika maeneo ya kusubiria usafiri wa umma.

Mbali na hayo, amesema mkoa pia unapanga kuweka mabango mawili makubwa ya kisasa ya matangazo, ambapo moja litajengwa katika eneo la Mzunguko wa Samaki. Mabango hayo yatatoa fursa kwa wananchi na wafanyabiashara wa Kigoma kutumia maeneo hayo kutangaza bidhaa, huduma na shughuli zao mbalimbali, huku yakiongeza mvuto wa mji.

Mhandisi Mweladzi amesema maboresho hayo yanaenda sambamba na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika mtandao wa barabara unaoiunganisha Kigoma na mikoa mingine nchini, akieleza kuwa kwa sasa usafiri umeendelea kuwa rahisi na wa haraka zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Amesema zamani safari kutoka Kigoma kwenda Kagera ilikuwa ikichukua muda mrefu na wakati mwingine siku nzima, lakini kutokana na maboresho ya barabara, kwa sasa safari hiyo inaweza kufanyika ndani ya takribani saa nne, huku barabara ya Kigoma hadi Dar es Salaam ikiwa imefanyiwa maboresho makubwa na sehemu kubwa ikiwa na lami.

Mhandisi Mweladzi amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa msukumo na kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Kigoma, akisema uwekezaji huo umeendelea kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, kuongeza usalama barabarani, kupendezesha mji na kuchochea shughuli za kiuchumi.