News

UWANJA WA NDEGE SHINYANGA KUCHOCHEA BIASHARA NA FURSA KWA WANANCHI

UWANJA WA NDEGE WA SHINYANGA KUCHOCHEA BIASHARA NA FURSA KWA WANANCHI

Shinyanga, 02 Sept, 2026

Uwanja wa Ndege wa mkoa wa Shinyanga kinatarajiwa kutumika kwa nyakati zote za mchana na usiku, baada ya kufungwa kwa taa zitakazomuongoza rubani. 

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Fredy Kipamila, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Kiwanja hicho, ambao umefikia asilimia 98 kwa miundombinu ya majengo na miundombinu mingine imefikia asilimia 100.

Mhandisi Kipamila amesema taa hizo zitafungwa hivi karibuni, ambapo tayari ujenzi wa barabara ya kutua na kuruka ndege yenye urefu wa Km 2.2 umekamilika kwa asilimia 100; yakiwemo maegesho ya ndege nne (4) aina ya Q400 Bombardier; barabara ya kuingia eneo la maegesho ya ndege, barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani yenye urefu wa Km. 1.8 na  maegesho ya magari 100 madogo na mabasi matatu (3) kutafungwa taa kwa ajili ya usalama kwa nyakati za usiku.

Amesema kwa sasa mkandarasi kampuni ya M/s China Henan International Cooperation Group Co Ltd (CHICO) wanaendelea na kukamilisha baadhi ya miundombinu kwenye jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja.

Mhandisi Kipamila amesema faida za kuwepo kwa kiwanja hiki kitaongeza ukuaji wa uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla kutokana na wafanyabiashara hususan wa madini na mazao mbalimbali ikiwemo pamba, na wagonjwa waliokuwa wakifuata matibabu nje ya mkoa huu sasa watakuwa wakitumia kiwanja hicho, tofauti na awali walikuwa wakitumia kiwanja cha ndege cha Mwanza na Tabora.

Aidha, ametaja faida nyingine iliyotokana na ujenzi wa kiwanja hicho kuwa ni kutoa ajira kwa wazawa asilimia 95 kati ya hizo asilimia 15 zilikuwa za wanawake; walioweza kujiongezea kipato na ujuzi wa kazi mbalimbali na watapewa vyeti maalumu kutambua mchango wao, jambo lililosaidia kupunguza uhaba wa ajira nchini.

Mhandisi Kipamila ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kutoa fedha za ujenzi wa kiwanja hiki, ambacho sasa kinakwenda kuwa mkombozi kwa watumiaji wake.

Wakati huo huo, Jengo la Kiwanja cha Ndege cha Mkoa wa Shinyanga, kwa kiwango cha Kimataifa, likiwa limesheheni miundombinu ya kisasa.

Mhandisi Mshauri, Yohana Mhando anayesimamia ujenzi wa mradi huo amesema jengo hilo litakuwa na chumba cha Rais, Watu Mashuhuri (VIP), eneo la wanaosafiri na wanaowasili, migahawa, zahanati, ofisi za watoa huduma mbalimbali ikiwemo za uuzaji wa tiketi, chumba cha ibada, chumba cha mapumziko kwa abiria wenye matatizo ya kiafya na chumba cha Wafanyabiashara Mashuhuri (CIP).

Mhandisi Yohana amesema pia kutakuwa na chumba kwa ajili ya faragha ya mtoto mdogo anayehudumiwa na mzazi au mlezi wake wakati wa kubadilishwa nguo.