News

TANROADS YAENDELEA NA MATENGENEZO YA BARABARA KUPUNGUZA FOLENI DAR ES SALAAM

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam inaendelea na ukaguzi na matengenezo ya barabara kuu pamoja na barabara zinazounganisha mitaa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa barabara zinazoendelea kufanyiwa ujenzi ni Goba–Matosa–Temboni yenye urefu wa kilomita saba, ambapo mradi huo unakamilisha awamu ya tatu kwa lengo la kuunganisha kilomita saba zilizobaki.

Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema, barabara hiyo inajengwa na mkandarasi mzawa, Kings Builders Tanzania na kwa sasa kazi imefikia hatua ya kuweka tabaka la C1, linalohusisha mchanganyiko wa kifusi na saruji.

Aidha amesema, ujenzi unaendelea pia katika barabara ya Kimara–Bonyokwa–Segerea–Kinyerezi yenye urefu wa kilomita saba, inayojengwa na mkandarasi mzawa kampuni ya Nyanza kwa gharama ya Shilingi bilioni 24.7.

"Barabara hii inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza msongamano, hususan kwa kuwawezesha wananchi wanaotoka Kinyerezi kusafiri kuelekea Morogoro kukatiza hadi Kimara bila kulazimika kupitia njia ndefu za Tabata au Mbezi." amesema

Katika eneo la Kinyerezi, Mhandisi Kyamba amesema, ujenzi wa daraja kubwa unaendelea na umefikia hatua ya maandalizi ya kujenga sakafu ya daraja (deck), hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya kukamilika kwa kiunganishi hicho muhimu cha barabara.

Katika hatua nyingine, amewataka wananchi na madereva kutumia barabara hizo kwa umakini, kuzingatia alama za usalama na kutoa nafasi kwa mitambo pamoja na magreda wakati kazi za ujenzi zikiendelea.

Vilevile ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha za kuboresha miundombinu na kutatua changamoto za barabara katika maeneo yenye milima, mabonde na udongo unaoteleza hususan barabara ya Goba hadi Matosa