News

BARABARA YA KAHAMA-BULYANHULU-KAKOLA KUUNGANISHA MANISPAA YA SHINYANGA NA MIKOA YA GEITA NA KAGERA

Shinyanga, 30 Agosti, 2026

Barabara ya Kahama-Bulyanhulu Junction - Kakola yenye urefu wa Km. 73 inayoendelea na utekelezaji wa ujenzi baada ya kukamilika inatarajiwa kuunganisha Manispaa ya Shinyanga na mikoa jirani ya Geita na Kagera. 

Mhandisi John Kalando, Msimamizi wa Kitengo cha Miradi ya Maendeleo cha Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Shinyanga, ametoa kauli hiyo wakati akitoa taarifa ya mradi huo wa kimkakati wa kiwango cha lami.

Aidha, amesema  ujenzi huo umeanzia eneo la Manzese - Kahama- Ilogi- Kakola Km. 73, ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 88.1 ikiwa tayari Km. 36.075  zimeshawekewa lami.

Mhandisi Kalando ameeleza faida za mradi huu wa kimkakati mara utakapokamilika kuwa utachochea maendeleo kupitia shughuli za kilimo, madini, ufugaji na mazao ya misitu.

Mradi huu unatekeleza na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa mgodi wa Barrick, ambapo ujenzi wa barabara hii iliyoanza tarehe 3 Juni, 2024 na kutarajiwa kukamilika Septemba 4, 2026; unasimamiwa na Mhandisi Mshauri kutoka TECU Shinyanga na kujengwa na Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kutoka China, ambaye amewasilisha maombi ya muda wa nyongeza, ambayo yapo katika hatua ya mapitio.

Barabara hii itafungwa taa 206 kwenye miji mikubwa ya Manzese, Karagwa, Ntobo, Segese, Lunguya, Ilogi, Kakola na Bugalawa, ambazo zitasaidia usalama nyakati za usiku na kuchochea maendeleo kwa shughuli za biashara; na taa hizo zitapendezesha miji hiyo.

Halikadhalika, Mhandisi huyo ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa rasilimali fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi hii, kwani kukamilika kwake kutachochea ukuaji wa sekta za madini, kilimo na ufugaji.

Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanatunza miundombinu saidizi kama taa za barabarani, alama za kuongoza magari na watembea kwa miguu, ili iwe na tija kwa maendeleo ya taifa.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Kalando, amesema serikali imeweza kulipa fidia ya jumla ya shilingi Milioni 408.3 kwa wananchi walioathirika kwa kupitiwa na ujenzi wa mradi wa barabara hiyo.

Amesema bado kiasi cha shilingi Milioni 5.5 za fidia kulipwa kutokana na migogoro ya kifamilia na pia kurekebisha majina yaliyokosewa katika kitabu.