News

DARAJA LA KAMISHANGO LABADILISHA MUONEKANO WA MULEBA

Kagera

Daraja la kisasa la Kamishango, lenye urefu wa mita 45, limejengwa pamoja na barabara ya maingilio yenye urefu wa kilomita 2 kwa kiwango cha lami. Daraja hilo limewekewa taa takribani 54, na hivyo kubadili mandhari ya Wilaya ya Muleba na kuongeza mvuto wa eneo hilo.

Daraja limejengwa kwa ustadi na kampuni ya DRK General Merchants Ltd, likiwa na njia ya watembea kwa miguu yenye urefu wa mita 90 pamoja na kingo za usalama wa barabara (guard rails) zenye urefu wa mita 2,000 kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watumiaji.

Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 100. Hata hivyo, mkandarasi anaendelea na kazi za usafi chini ya daraja kwa kuondoa udongo na takataka zilizobaki kutokana na shughuli za ujenzi, ili kuhakikisha maji yanapita vizuri.

Daraja hilo limeboresha mawasiliano ya barabara inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya ya Muleba na miji midogo ya kibiashara ya Nshamba, Kishanda, Buganguzi na Kamachumu. Pia limechochea shughuli za kiuchumi na kurahisisha usafirishaji wa abiria, mazao ya chakula na bidhaa za biashara.

Aidha, uwekaji wa taa, alama za usalama na guard rails umeongeza usalama kwa watumiaji wa barabara, huku daraja hilo likibadilisha mandhari ya eneo na kuongeza mvuto wa Muleba.