News

KUTOKA HOFU YA MITUMBWI HADI UHURU WA DARAJA: KYANYABASI YAPATA MWANGA MPYA

Kagera

Bukoba, Kagera -  Kwa muda mrefu, kuvuka eneo la Kyanyabasi haikuwa safari ya kawaida kwa wananchi wa Tarafa ya Katerero. Ilikuwa ni safari iliyohitaji tahadhari, uvumilivu na wakati mwingine kusubiri hadi huduma ya kivuko ipatikane.

Leo, hali hiyo inaanza kubadilika. Kukamilika kwa Daraja la Kyanyabasi lenye urefu wa mita 105 na maingiliano ya mita 600 kumeleta matumaini mapya kwa wananchi ambao sasa wanaweza kuvuka kwa urahisi zaidi na kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Proges Mtuli, mkazi wa Kata ya Kishogo, anasema changamoto za zamani bado ziko kwenye kumbukumbu za wananchi, hasa kipindi ambacho walilazimika kutumia mitumbwi iliyokuwa ikihudumia idadi kubwa ya watu.

Anasema wakati mwingine hali hiyo ilisababisha hofu na usumbufu, huku kuanzishwa kwa kivuko baadaye kukisaidia kupunguza baadhi ya changamoto lakini kukawa na mipaka ya muda wa huduma na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya wananchi.

Kwa Mtuli, daraja si tu njia ya kuvuka maji, bali ni fursa mpya kwa jamii.

Anasema urahisi wa usafiri utawezesha wananchi kusafirisha mazao, bidhaa za biashara na kwenda katika maeneo mbalimbali kwa ufanisi zaidi, jambo linaloweza kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Pamoja na mafanikio hayo, wananchi wameomba taa zaidi ziongezwe katika barabara hususan maeneo ya nje ya daraja, ili kuongeza usalama wa watumiaji wakati wa usiku.

Wakati huo huo, wameahidi kuwa sehemu ya jukumu lao ni kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa na kutunzwa ili iendelee kutoa huduma kwa vizazi vijavyo.

Daraja la Kyanyabasi sasa linafungua ukurasa mpya kwa Katerero - ukurasa unaotarajiwa kuleta usafiri wenye uhakika zaidi, kurahisisha biashara na kuunganisha wananchi na fursa za kiuchumi kwa urahisi zaidi.