Tabora, 26 Agosti, 2026
Mtandao mkubwa wa barabara kwa mkoa wa Tabora, ambao unajumla ya Kilometa 2,188.09 umekuwa kichocheo kikuu cha kukuza uchumi wa Taifa, kwa kuwa na usafiri na usafirishaji wa uhakika.
Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji amesema mkoa huu unaongoza kwa kuwa na mtandao mkubwa wa barabara Kuu zenye jumla ya Km. 1,077.12 na Km 1,073.37 ni za Barabara za Mkoa kati ya hizo Km. 44.5 ni za lami huku Km 1,028 ni kiwango cha changarawe.
Barabara ya Wilaya ni Km 36.4 kati ya hizo Km. 4 ni za lami na zilizobakia ni za changarawe.
Aidha, jumla ya Km 804.65 za barabara kuu ni za kiwango cha lami na Km 273.6 ni za changarawe (Ikwele - Rungwa; na Tabora-Mambali- Mkurudede kupitia Bukumbi); kwa barabara za mkoa Km 44.75 ni za lami na Km 1,028.62 ni za changarawe au udongo na Km 4.00 ni za kiwango cha lami kwa barabara za wilaya (barabara ya Igunga – Mbutu) na km 33.60 ni za changarawe au udongo kwa barabara za wilaya zilizokasimiwa kwa wakala ya barabara katika mkoa wa Tabora.
Aidha, mtandao huo umekuwa ukirahisha usafiri a usafirishaji kwa kuunganisha mkoa wa Tabora na wilaya zake, pamoja na mikoa jirani.
Mhandisi Mlimaji, amesema pia mkoa wa Tabora unahudumia jumla ya madaraja 677 yaliyojengwa kwenye mtandao huo, ambayo ni Kizengi na Nyahua (yapo katika barabara ya kutoka Tabora-Manyoni-Dodoma); wakati madaraja ya Wala na Kasisi (yapo kwenye barabara ya Tabora-Mpanda) na Mto Koga (Tabora-Katavi).
Amewatoa hofu watumiaji wa barabara kwenye mkoa kwa sasa hakuna tatizo lenye kusababisha barabara kujifunga nyakati za mvua, kutokana na madaraja hayo yamekuwa mkombozi kwa kuweza kupitisha maji mengi kwa wakati, tofauti na madaja yaliyokuwa awali yalikuwa madogo na kufanya maji kupita juu na kusababisha mafuriko.