Dar es Saalam
Mradi wa BRT1 unaotekelezwa kati ya Ubungo na Kimara umefikia asilimia 82 ya utekelezaji, ukiwa na lengo la kuboresha miundombinu, kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa usafiri.
Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Agness Mwakabende, amesema kazi ya uwekaji wa tabaka la mwisho la lami katika eneo hilo inakaribia kukamilika. Kukamilika kwake kutawezesha kuwa na jumla ya njia tatu za magari katika kila upande, hatua inayotarajiwa kuboresha mtiririko wa magari.
Mhandisi Mkazi wa BRT1 Package A, Girma Haile, amesema mradi unahusisha ukarabati wa njia zilizopo za magari mchanganyiko na kuongeza njia ya tatu katika kila upande, kuanzia Ubungo hadi takribani mita 600 baada ya Daraja la Kimara.
Aidha, mradi unahusisha ujenzi na uboreshaji wa njia za watembea kwa miguu na waendesha baiskeli, pamoja na vituo vipya vya mabasi katika maeneo mbalimbali.
Mhandisi wa Usafirishaji kutoka CRBC, Flavius Matata, amesema katika hatua za mwisho mkandarasi anaendelea na maandalizi ya uwekaji wa alama za barabarani na miundombinu mingine ya usalama.
Watumiaji wa barabara wameombwa kuendelea kufuata alama na maelekezo ya waelekezaji wa magari, pamoja na kuchukua tahadhari wanapopita katika maeneo yenye shughuli za ujenzi.
Wahandisi wamewashukuru Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi, TANROADS na Benki ya Dunia kwa ushirikiano na mchango wao katika utekelezaji wa mradi.