News

TANROADS YAJENGA JENGO LA KISASA LA ABIRIA KIWANJA CHA NDEGE CHA TABORA

Tabora, 25 Agosti, 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imejivunia kwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa ukarabati na uboreshaji wa Kiwanja cha ndege cha mkoa wa Tabora, ambapo kumejengwa jengo kubwa la kisasa la abiria ukilinganisha na jengo la zamani lililokuwa dogo.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji, aliyekuwa akielezea hatua za utekelezaji wa ujenzi wa Kiwanja hicho, ambapo amesema tayari utekelezaji wa ujenzi jengo la abiria umefikia asilimia 99 za utekelezaji wake.

Mhandisi Mlimaji amesema jengo hilo la kisasa lina mita za mraba 4,560 litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria mia moja na ishirini (120) kwa wakati mmoja, ambapo watumiaji watakuwa na uwezo wa kukaa kwenye viti bora na vya kisasa; pia ujenzi wa ofisi za idara mbalimbali na sehemu za biashara yakiwemo maduka na migahawa.

Amesema pia jengo hilo litakuwa na mifumo mbalimbali ya kiuendeshaji zikiwemo televisheni zilizofungwa kwa ajili ya kutoa taarifa na matangazo mbalimbali yakiwalenga watumiaji, mfumo wa viyoyozi, mkanda wa kwa ajili ya mizigo ya abiria wanaowasili na wanaondoka, na mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo yao, na mfumo wa kamera za kufuatilia nyendo mbalimbali za kiusalama.

Mbali na ujenzi wa jengo hilo pia TANROADS imekamilisha ujenzi wa barabara za kuingia na kutoka kwenye kiwanja hicho kwa kiwango cha lami yenye urefu wa mita 675, pia ujenzi wa uzio wa usalama wenye urefu wa Km. 6.25, sambamba na ujenzi wa mifereji ya kupitisha maji hususan ya mvua; na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Hali ya Hewa; ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege; jengo la kituo cha umeme wa dharura lenye majenereta mawili yenye umeme wa 1000KvA na 40KvA (power station) na pia umeme wa kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kufungwa transfoma la 1250KvA (primary 11Kv to secondary 400V).

Pia ujenzi huo umehusisha ujenzi wa eneo la maegesho ya magari lenye mita za mraba 1,668 litaegesha magari yapatayo 54; usimikaji wa taa zenye kutumia mfumo wa umeme jua katika barabara ya kuingia na kutoka kiwanjani; halikadhalika maegesho ya ndege yenye uwezo wa kuegesha ndege kubwa nne aina ya Bonderdier.

Amesema kazi hizi zimefanywa na mkandarasi Kampuni ya M/s Beijing  Construction Engineering Group Co Ltd ya China, ambapo walipewa mua wa mwaka mzima wa uangalizia kuanzia tarehe 17 Oktoba, 2025 ambao unaendelea hadi tarehe 17 Oktoba, 2026, na ukaguzi wa mwisho kabla ya kukabidhiwa mradi ni tarehe 22 Oktoba, 2026.

Mhandisi Mlimaji amesema ujenzi wa jengo hili unafaida kubwa ikiwemo ya kurahisha usafiri wa anga kwa wakazi wa mkoa wa Tabora na mikoa jirani; kurahisisha shughuli za kibiashara; Kurahisisha usafiri kwa watafiti wa kilimo na mbegu wanaofanya tafiti mbalimbali, pia kukuza uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla kwa idadi kubwa ya wasafiri wakiwemo watalii, pia faida nyingine ni kuwa usafiri wa anga ndio usafiri salama na uhakika kushinda nyingine zote kutokana na kutokuwa na ajali za mara kwa mara.

Ametoa wito kwa watumiaji wa Kiwanja hicho kuhakikisha wanatunza miundombinu na thamani zilizopo hapo, ili jengo hili liweze kudumu kwa kutumia na vizazi vya sasa na vijavyo kwa muda mrefu.

Ameishukuru serikali kwa ujenzi wa kiwanja hiki cha ndege, ambacho sasa kinakwenda kuwa mkombozi kwa watumiaji wa usafiri wa anga kwa mkoa wa Tabora, mikoa ya jirani na hata nchi jirani.