UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI WAFIKIA ASILIMIA 41, KAZI ZASONGA KWA KASI
DAR ES SALAAM:
Ujenzi wa Daraja la Jangwani umefikia asilimia 41, huku kazi mbalimbali zikiendelea katika eneo la mradi kwa lengo la kukamilisha kwa wakati miundombinu hiyo muhimu ya usafiri jijini Dar es Salaam.
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa karibu, kuhakikisha kazi zinazotekelezwa zinaendelea kwa kasi, ubora na kuzingatia viwango vilivyowekwa.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Meneja wa Mradi, Mhandisi Leonard Ngayungi, amesema hatua iliyofikiwa inaonesha kasi ya utekelezaji wa mradi, huku kazi zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya daraja.
Amesema ziara hiyo imejikita katika kutathmini kazi zinazotekelezwa katika maeneo ya mradi, kutatua changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha shughuli za ujenzi zinaendelea kwa ufanisi na kwa kuzingatia ratiba ya utekelezaji
“Kwa sasa mradi umefikia asilimia 41 ya utekelezaji na kazi zinaendelea katika maeneo mbalimbali.
Tunaendelea kusimamia kwa karibu hatua zote za ujenzi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika,” amesema Mhandisi Ngayungi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Ngayungi, Daraja la Jangwani lenye urefu wa mita 390 ni sehemu muhimu ya kuboresha miundombinu ya usafiri katika eneo hilo, ambapo kukamilika kwake kutasaidia kuimarisha usafiri na usalama kwa watumiaji wa barabara.
Amesema TANROADS itaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mradi huo kwa karibu, ikiwemo kushughulikia changamoto zinazojitokeza wakati wa ujenzi, ili kuhakikisha kazi zinaendelea na mradi unafikia malengo yaliyokusudiwa