WANANCHI WAHIMIZWA KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA KWA MAENDELEO ENDELEVU
Dodoma, 29 Julai, 2026
Wananchi wanaoishi karibu na miundombinu ya barabara na madaraja nchini wamehimizwa kuitunza na kuilinda ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Geofrey Kasekenya, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja jijini Dodoma.
Mhandisi Kasekenya amesema kuwa barabara na madaraja ni mali ya umma, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kuvilinda na kuacha vitendo vinavyosababisha uharibifu wa miundombinu hiyo.
Ameeleza kuwa baadhi ya vitendo kama kupitisha mifugo, ikiwemo ng'ombe, juu ya barabara na kung'oa alama za barabarani ni uharibifu unaoisababishia Serikali gharama za ziada za matengenezo ambazo zingeweza kuepukika.
"Niwaombe wananchi watambue kuwa barabara hizi si mali ya Serikali pekee, bali ni mali ya umma.
Kila mmoja ajione kuwa ni sehemu ya jukumu la kuzilinda, kwani miundombinu hii inawanufaisha wananchi wote," amesema Mhandisi Kasekenya.
Aidha, amesisitiza kuwa kuondoa au kuharibu alama za barabarani kunaweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara kwa kuwa alama hizo hutoa mwongozo muhimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara, hivyo kuongeza hatari ya ajali.