News

NAIBU WAZIRI UJENZI APONGEZA KAZI NZURI YA UJENZI WA MADARAJA DODOMA

NAIBU WAZIRI UJENZI APONGEZA KAZI NZURI YA UJENZI WA MADARAJA DODOMA

Dodoma, 27 Julai, 2026

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Geofrey Kasekenya amepongeza kazi kubwa na nzuri inayoendelea kufanywa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ya ujenzi wa miundombinu ya madaraja kwenye barabara ya Ntyuka - Kikombo mkoani Dodoma.

Mhandisi Kasekenya ametoa pongezi hizo hivi karibu alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya mkoa wa Dodoma, lakini ametoa angalizo la ujenzi huo kujengwa kwa haraka kutokana na kuwa na kipaumbele kikubwa.

Amesema kuwa barabara hii ni muhimu mbali na kutumika na wananchi, pia ndio barabara kuu inayotumika na watumishi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wanapokwenda kazini.

“Viongozi wengi wanatamani hii barabara ikamilike kwa wakati ili waweze kufika maeneo ya kazi katika mazingira salama, na pia hii barabara ndio inaunganisha vijiji vya Mapinduzi, Mahona,hadi Ntyuka, pia inapunguza adha kwa wanaokwenda Mvumi,” amesema Mhandisi Kasekenya.

Hatahivyo, ametoa maelekezo kwa wasimamizi na mkandarasi kampuni ya CHICCO kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa madaraja hayo makubwa ya MGR, SGR na mengine katika barabara hiyo kabla ya mvua kuanza, ili kuwaondolea adha na kikwazo kwa watumiaji wa njia hiyo kwa kushindwa kupita kutokana na maji kujaa eneo wanalopita sasa.

Amesema kwa mujibu wa makubaliano ya kati ya msimamizi na Mkandarasi, wamemhakikishia kuwa madaraja yote yatakamilika mwezi Septemba 2026, ikiwa bado ni majira ya kiangazi.

Halikadhalika, amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa madaraja hayo na barabara unganishi zitasimikwa taa zitakazoongeza usalama kwa watumiaji na pia kupendezesha maeneo hayo, na kuchochea uchumi kwa wakazi kuendelea na shughuli zao za biashara hata nyakati za usiku.

Hatahivyo, amemhakikishia mkandarasi kuwa serikali inashughulikia madai yao na yaliyopo yatalipwa kwa wakati.

Awali Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani alimweleza Naibu Waziri kuwa barabara hii ya kutoka Ntyuka - Mvumi - Kikombo inaurefu wa Km. 76, ambapo serikali ilianza kutekeleza mradi huu wa ujenzi kwa awamu, ikiwemo ya ujenzi wa madaraja makubwa manne na barabara yenye kiwango cha lami Km. 16.4 ikiwa ni upande wa Kikombo na Km. 8.6 upane wa Ntyuka.