AHADI YA WAZIRI ULEGA YATIMIA, UDSM SASA YANG'AA USIKU KWA USALAMA WA WANAFUNZI PAFUNGWA TAA 41
Dar es Salaam, 15 Julai, 2026
Ahadi iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), ya kufunga taa za barabarani katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sasa imetekelezwa, hatua inayoongeza usalama wa wanafunzi, wahadhiri na watumiaji wengine wa barabara nyakati za usiku.
Mhe. Ulega alitoa ahadi hiyo mwezi Februari, 2026 alipokutana na wanafunzi wa Kada ya Uhandisi wa UDSM.
Katika mkutano huo, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye, aliwasilisha changamoto mbalimbali zilizokuwa zikilikabili chuo, ikiwemo ukosefu wa taa za barabarani uliosababisha giza na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na watumiaji wengine wa barabara usiku.
Akijibu hoja hiyo, Waziri alimhakikishia Makamu Mkuu wa Chuo kuwa Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) itafunga taa za barabarani ili kuboresha usalama na mazingira ya kujifunzia chuoni.
Ahadi hiyo sasa imetekelezwa ambapo jumla ya taa 41 zimesimikwa katika mtandao wa barabara wa UDSM wenye urefu wa kilomita 12.11, na kufanya mazingira ya chuo kuwa salama na yenye mwanga wakati wa usiku. Aidha, tathmini ya maeneo mengine imekamilika na imebainika kuwa kuna uhitaji wa zaidi ya taa 400 ili kukidhi mahitaji ya mtandao mzima wa barabara chuoni.
Wanafunzi wameeleza kufurahishwa na muonekano mpya wa chuo, hususan katika kipindi hiki wanapohitimisha mitihani ya muhula, wakisema mwanga huo umeongeza usalama na kuwawezesha kufanya shughuli za masomo na utafiti kwa utulivu hata nyakati za usiku.
Mbali na ahadi ya kufunga taa, Mhe. Ulega pia alitangaza zawadi ya shilingi milioni 10 kwa mwanafunzi atakayewasilisha andiko bora lenye suluhisho la kupunguza foleni nchini, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ubunifu wa vijana katika kutatua changamoto za maendeleo.
Utekelezaji wa mradi huu unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua kwa vitendo kupitia utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii.