News

ENG. KASEKENYA AITAKA TANROADS KUSHIRIKIANA NA WADAU KUTUMIA HUDUMA ZA MAABARA

ENG. KASEKENYA AITAKA TANROADS KUSHIRIKIANA NA WADAU KUTUMIA HUDUMA ZA MAABARA

Dodoma, 15 Julai, 2026

NAIBU Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, amezungumzia umuhimu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kuitangaza kwa  kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za elimu ya uhandisi katika kuendesha maabara zake za kisasa.

Hatua hiyo itaiwezesha TANROADS kuongeza mapato, kuimarisha huduma za kitaalamu na kuifanya taasisi hiyo kuwa kitovu cha umahiri katika upimaji wa malighafi za  ujenzi wa barabara nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.

Mhandisi Kasekenya amesema hayo leo tarehe 15 Julai, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu ya TANROADS iliyopo maeneo ya Njedengwa jijini Dodoma.

Ameitaka taasisi hiyo kuhakikisha viongozi wake wakuu na watumishi wanaopaswa kuhamia Makao Makuu ya nchi wanakamilisha uhamisho wao ifikapo mwisho wa Agosti mwaka huu.

Amemtaka Mkandarasi kampuni ya CRJE East Africa Ltd anayejenga jengo hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85 kuongeza kasi ili likamilike kwa wakati.

"Tunapoelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ni muhimu taasisi za umma kuangalia namna ya kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza tija kwa umma hivyo TANROADS ina maabara za kisasa, ambazo zinaweza kutumika kutoa huduma za kibiashara na kitaalamu kwa taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi," amesisitiza Naibu Waziri Mhandisi Kasekenya.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo utaifanya TANROADS kuwa kituo cha umahiri katika upimaji wa vifaa vya ujenzi wa barabara na kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani kupitia ubadilishanaji wa uzoefu na teknolojia.

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Naibu Waziri alisema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa baada ya kupata maelezo kutoka kwa mshauri elekezi wa Serikali, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), pamoja na TANROADS kama watumiaji wa majengo hayo.

Alisema jengo la maabara (Road Development Unit – RDU), ambalo pia litatumika kama ofisi za watumishi, linatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa Agosti na kuanza kutumika mara moja, huku jengo kuu la Makao Makuu ya TANROADS likitarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu kutokana na kuchelewa kuwasili kwa baadhi ya vifaa maalumu vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi.

"Nimeelezwa kuwa baadhi ya viongozi tayari wameanza kufanya kazi katika jengo la maabara, maelekezo yangu ni kwamba ifikapo mwisho wa Agosti viongozi wote wahamie Dodoma ili wawe sehemu moja, wafanye maamuzi kwa pamoja na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao," alisema Mhandisi Kasekenya.

Aidha, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa, akisema uwekezaji huo unaimarisha uwezo wa taasisi za Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, alisema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya CRJE East Africa Limited chini ya usimamizi wa Tanzania Building Agency (TBA) katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 78,474.

Alisema ujenzi ulianza Februari 1, 2024 na kwa sasa umefikia asilimia 85, huku jengo kuu likiwa limekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na kazi nyingi zilizobaki zikiwa ni za umaliziaji.

Mhandisi Zuhura alisema tayari takribani watumishi 220 wa TANROADS wamehamia Dodoma kufuatia utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhamishia taasisi zake Makao Makuu ya nchi.

Aliongeza kuwa mradi huo umechangia matumizi ya malighafi zinazozalishwa nchini, hatua iliyonufaisha viwanda vya ndani, huku ukitoa ajira 211 kwa Watanzania na ajira kwa wataalamu wanane kutoka nje ya nchi.

Kuhusu changamoto zilizojitokeza, alisema kuchelewa kupatikana kwa baadhi ya vifaa vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi kulichelewesha baadhi ya kazi, lakini kwa sasa vifaa vingi vimewasili na utekelezaji unaendelea kwa kasi.

Akihitimisha ziara hiyo, Mhandisi Kasekenya aliwataka watumishi wa TANROADS kufanyakazi kwa  uadilifu na uwajibikaji ili kuhakikisha barabara zinazojengwa nchini zinakuwa na viwango na ubora unaostahili na zinadumu kwa muda mrefu.

Pia amewataka watumishi kuzitangaza maabara hizo kwa wadau ili waweze kuzitumia.kwa kupima ubora wa malighafi wanazozitumia katika majenzi mbalimbali.

"Hatuwezi kuwa na maabara za kisasa halafu tukashuhudia barabara zikiharibika muda mfupi baada ya kujengwa, uadilifu na uwajibikaji ndiyo msingi wa kulinda ubora wa kazi na thamani ya fedha za umma," alisema.