WATAALAM WA TANROADS KUANZA UKAGUZI WA BARABARA
Morogoro, 12 Julai, 2026Wataalam kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), wanatarajia kuanza ukaguzi wa barabara kwa kutumia mtambo mpya wa kisasa baada ya kufuzu mafunzo mkoani Morogoro.
Meneja wa Usimamizi wa Samani za Barabara wa TANROADS, Mhandisi Leonard P. Mombia amesema baada ya mafunzo hayo ya nadharia na vitendo, sasa wataalam hao wataingia barabarani kuanza ukaguzi wa kina na baadaye kuwasilisha ripoti, itakayosaidia utekelezaji wa matengenezo ya barabara katika maeneo yatakayobainishwa na mtambo.
Amesema katika mafunzo ya vitendo waliweza kukagua barabara kuu ya TANZAM kuanzia maeneo ya Msamvu hadi Iyovi na kukusanya taarifa za hali halisi ya barabara hiyo.
Mhandisi Mombia amesema sasa wataalam wapo tayari kwa ukaguzi utakaoanzia katika barabara kuu ya TANZAM (Dar es Salaam hadi Tunduma); barabara ya Chalinze - Arusha hadi Namanga; pia barabara ya Morogoro - Dodoma - Singida - Tabora mpaka Mwanza.
Amezitaja barabara kuu nyingine zitakazojumuishwa katika zoezi hilo la ukaguzi kuwa ni kuanzia Iringa - Dodoma mpaka Manyara; na pia barabara ya Tabora kwenda Kigoma.