MANDHARI YA KUVUTIA YA KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA CHA MSALATO
Dodoma, 12 Julai, 2026
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kinaendelea kung'ara huku ujenzi wake ukifikia asilimia 87.97 kwa miundombinu na asilimia 76.15 kwa majengo, kikionesha taswira ya kisasa inayotarajiwa kubadilisha sekta ya usafiri wa anga nchini.
Jengo la abiria litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka na litakuwa na lifti, eskaleta, mifumo ya kisasa ya usalama, maeneo ya ibada, sehemu za watoto, migahawa, maduka mbalimbali pamoja na huduma za kifedha ili kuwapa wasafiri huduma bora na za viwango vya kimataifa.
Kiwanja hicho kitakuwa na maegesho ya magari 500, maegesho ya ndege yanayoweza kupokea ndege kubwa ikiwemo Boeing 777 na Airbus, barabara ya kuruka na kutua yenye urefu wa kilomita 3.6, pamoja na mnara wa kuongozea ndege wenye urefu wa mita 56.2.
Mradi huu unatarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kwa kuimarisha biashara, utalii, uwekezaji na usafiri wa anga, huku ukiifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha usafiri wa kimataifa.