WATAALAMU WA TANROADS WAISHUKURU SERIKALI KWA KUNUNUA MTAMBO WA KISASA WA UKAGUZI WA BARABARA
Morogoro, 08 Julai, 2026
Wataalamu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) wameishukuru Serikali kwa kununua mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa barabara, wakisema utaongeza ufanisi katika ukaguzi, upangaji wa matengenezo na uhifadhi wa miundombinu ya barabara.
Mhandisi Magnus Mutayoba kutoka Kitengo cha Samani za Barabara TANROADS Makao Makuu amesema mtambo huo utasaidia kubaini kwa haraka uharibifu wa barabara ikiwemo mashimo na nyufa, pamoja na kufanya ukaguzi wa barabara mpya kabla ya kukabidhiwa Serikali ili kuhakikisha zinakidhi viwango vilivyowekwa kwenye mikataba.
Kwa upande wake, Mhandisi Richard Mhagama kutoka TANROADS Mkoa wa Morogoro amesema mtambo huo hukusanya taarifa nyingi kwa muda mfupi, jambo litakalowezesha kupanga bajeti za matengenezo kwa kuzingatia hali halisi ya barabara badala ya makadirio ya awali.
Naye Mhandisi Elina Kyando kutoka TANROADS Mkoa wa Shinyanga amesema mafunzo waliyopata yatawawezesha kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa ufanisi zaidi na kusaidia kuhifadhi barabara kwa muda mrefu.
Ameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo, akieleza kuwa mtambo huo una uwezo wa kukagua zaidi ya kilometa 200 za barabara kwa muda mfupi, hivyo kuongeza kasi na ubora wa kazi za ukaguzi nchini.