News

MTAMBO WA KISASA WA TANROADS KUINUA VIWANGO VYA USALAMA WA BARABARA NCHINI

MTAMBO WA KISASA WA TANROADS KUINUA VIWANGO VYA USALAMA WA BARABARA NCHINI

Morogoro, 08 Julai, 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza kutumia mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa barabara utakaowezesha kutathmini kiwango cha usalama wa barabara na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kwa usahihi zaidi.

Meneja wa Kitengo cha Usalama Barabarani TANROADS, Mhandisi George Daffa amesema mtambo huo hukusanya na kuchakata taarifa mbalimbali za barabara ili kuzipangia hadhi ya usalama kuanzia nyota moja hadi nyota tano kulingana na viwango vya kimataifa.

Amesema barabara yenye hadhi ya nyota tano hukidhi vigezo vya usalama kwa watumiaji wote, ikiwemo uwepo wa njia za watembea kwa miguu, vivuko salama, njia za baiskeli, mabega ya barabara, alama za barabarani na mistari ya usalama.

"Kwa kutumia mtambo huu, tunaweza kutambua kwa usahihi maeneo yenye changamoto za usalama na kutoa mapendekezo ya maboresho kabla hayajasababisha ajali au uharibifu mkubwa," amesema Mhandisi Daffa.

Ameongeza kuwa mtambo huo pia hukusanya taarifa kuhusu upana wa barabara, mabega, alama, mistari, nyufa, mikunjo na vipengele vingine muhimu vinavyosaidia kupanga matengenezo kwa kuzingatia taarifa halisi badala ya makadirio.