MTWARA WANUFAIKA NA UWEKEZAJI MIKUBWA WA BARABARA
Mtwara, 05 Julai, 2026
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema ujenzi unaoendelea wa barabara za mikoa ya Kusini mwa Tanzania ni ushahidi mwingine wa matumizi mazuri ya fedha ambazo nchi imekopa kwa wahisani.
Waziri Ulega ametoa kauli hiyo alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya kilometa 160 kati ya Mnivata – Newala – Masasi inayojengwa kwa kiwango cha lami na kuongeza kuwa mikopo nafuu inayochukuliwa na Serikali inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
“Matokeo ya utekelezwaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara ambayo hurahisisha usafiri, kuchochea biashara, kuimarisha harakati za maendeleo ni ushahidi wa wazi wa namna matumizi ya fedha za mikopo yanavyoleta matokeo chanya kwa wananchi wote, nchi nzima”, amesema Ulega.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Ulega amesema mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa iliyonufaika zaidi na uwekezaji wa Serikali katika sekta ya barabara, ukishika nafasi ya tatu kwa kutanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.
"Dar es Salaam ndiyo mkoa uliopata fedha nyingi zaidi kwa sababu ni mkoa wa Watanzania wote na Dodoma imefuata kwa kuwa ni makao makuu ya nchi. Baada ya Dar es Salaam na Dodoma, kunakofuata ni Mtwara, “ amefafanua Ulega.
Akielezea umuhimu wa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi, Waziri Ulega amesema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa kutokana na usafirishaji mkubwa wa zao la korosho ambapo zaidi ya nusu ya korosho zinazozalishwa nchini husafirishwa kupitia barabara hiyo.
Naye Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota amewahimiza wananchi kuonesha ushahidi wa barabara hiyo na kueleza umuhimu wake kwa maendeleo yao badala ya kukubali kupotoshwa na kauli zinazodai kuwa fedha za mikopo ya maendeleo hazijulikani zilikoelekezwa.
“Mkopo wa zaidi ya Shilingi bilioni 230 kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) umeelekezwa katika ujenzi wa barabara ya Mnivata – Newala – Masasi, jambo linalodhihirisha wazi matumizi ya fedha hizo na Serikali ya Rais Samia inakopa kwa kujua fedha zinakoenda hivyo wakija, waonesheni barabara hii. Huu ndiyo ushahidi wa fedha za mkopo zinavyotekeleza maendeleo," amesema Ulega.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini Rashid Mtima amesema wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanathamini hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza ndoto ya muda mrefu ya kuboresha mtandao wa barabara mkoani humo.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo umeleta matumaini mapya kwa wananchi na kufungua fursa za kiuchumi kupitia usafirishaji wa watu na bidhaa.