News

MZANI WA MIKUMI WAFANYIWA MATENGENEZO YA KUONDOA MATOPE

MZANI WA MIKUMI WAFANYIWA MATENGENEZO YA KUONDOA MATOPE

Morogoro, 4 Julai 2026

Mzani wa kupima magari ya mizigo wa upande wa Kaskazini wa Mikumi, mkoani Morogoro, unafanyiwa matengenezo ya kuondoa matope na uchafu mwingine ulioingia wakati wa msimu wa mvua.

Msimamizi wa zamu wa mzani huo, Bi. Rosemary Thomas, amesema matengenezo hayo hufanyika kila baada ya miezi mitatu ili kuzuia hitilafu zinazoweza kusababishwa na uchafu unaojikusanya chini ya mzani. 

Bi. Rosemary amesema kuwa, pamoja na kufungwa kwa njia moja ya mzani kwa ajili ya matengenezo, huduma zinaendelea kutolewa kupitia upande wa Kusini. Amefafanua kuwa si magari yote hupimwa uzito, bali ni yale yanayopewa ishara ya taa nyekundu, huku mengine yakiruhusiwa kuendelea na safari kwa kuwa mzani huo una njia mbili, ikiwemo inayopima magari yakiwa yanaendelea kutembea.

"Matengenezo haya ni ya muda mfupi na hayaathiri utoaji wa huduma. Upande mwingine unaendelea kutoa huduma, hivyo hakuna msongamano wa magari kwa kuwa yale yasiyopewa ishara ya kuingia mzani yanaendelea na safari," amesema Bi. Rosemary 

Athari kwa jamii:

Matengenezo hayo yanahakikisha huduma za upimaji zinaendelea kwa ufanisi, hupunguza usumbufu kwa wasafirishaji na wananchi, na kusaidia kulinda miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha magari yanazingatia viwango vya uzito vinavyoruhusiwa.

Mzani wa Mikumi ni miongoni mwa mizani yenye matumizi makubwa nchini, ukihudumia magari ya mizigo yanayosafiri kati ya Morogoro na mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara pamoja na mikoa mingine.