News

MZANI WA MIKUMI WAFANYIWA MATENGENEZO KINGA

MZANI WA MIKUMI WAFANYIWA MATENGENEZO KINGA

Morogoro, 4 Julai 2026

Mzani wa kupima magari ya mizigo wa upande wa Kaskazini wa Mikumi, mkoani Morogoro, unafanyiwa matengenezo kinga yanayohusisha kuondoa matope, takataka, kuweka grisi kwenye sensa na kukagua hali ya vipuri.

Msimamizi wa zamu wa mzani huo, Bi. Rosemary Thomas, amesema matengenezo hayo hufanyika kila baada ya miezi mitatu ili kuzuia hitilafu zinazoweza kujitokeza pasipo kutarajia na kuhakikisha mzani unakuw akatik ahali nzuri wakati wote wa upimaji. 

Bi. Rosemary amesema kuwa, pamoja na kufungwa kwa njia moja ya mzani kwa ajili ya matengenezo, huduma zinaendelea kutolewa kupitia upande wa Kusini. Amefafanua kuwa si magari yote hupimwa uzito, bali ni yale yanayopewa ishara ya taa nyekundu, huku mengine yakiruhusiwa kuendelea na safari kwa kuwa mzani huo una njia mbili, ikiwemo inayopima magari yakiwa yanaendelea kutembea.

"Matengenezo haya ni ya muda mfupi na hayaathiri utoaji wa huduma. Upande mwingine unaendelea kutoa huduma, hivyo hakuna msongamano wa magari kwa kuwa yale yasiyopewa ishara ya kuingia mzani yanaendelea na safari," amesema Bi. Rosemary 

Athari kwa jamii:

Hakuna athari yeyote ya utoaji huduma kwa jamii kwani, matengenezo hayo yanahakikisha huduma za upimaji zinaendelea kwa ufanisi kwa kutumia mzani wa Kusini na mifumo ya mzani inayopima magari yakiwa kwenye mwendo, hivyo hupunguza usumbufu kwa wasafirishaji na wananchi pindi zoezi hilo likiendelea, na kusaidia kulinda miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha magari yanazingatia viwango vya uzito vinavyoruhusiwa.

Mzani wa Mikumi ni miongoni mwa mizani yenye matumizi makubwa nchini, ukihudumia magari ya mizigo yanayosafiri kati ya Morogoro na mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Lindi, Mtwara pamoja na nchi jirani za Zambia, Kongo na Malawi.