News

SERIKALI KUONGEZA KASI  UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO 

SERIKALI KUONGEZA KASI  UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO 

Mara, 03 Julai, 2026

Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu  Lameck Nchemba amesema Serikali imejipanga kufanya kazi ili kuhakikisha inatekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara katika Mikoa na Wilaya zote nchini 

Akizungumza  katika mkutano wa hadhara Wilayani  Butiama mkoani Mara, l  Dkt.Mwigulu amesema Serikali ilifanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kielelezo  yenye mahitaji kwa nchi nzima ikiwemo Daraja la Kigongo- Busisi ambapo ilitekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.

Dkt.Mwigulu amesema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuongeza kasi katika utekelezaji wa miundombinu wezeshi ndani ya Mikoa na Wilaya ambapo ameelekeza usanifu wa barabara ya Kitaramanka-Magunga-Busegwe km 37 kuanza haraka na barabara zote za mkoa wa Mara kuwekwa katika utaratibu wa utekelezaji.

“Niwahakikishie Serikali  imejipanga  kuhakikisha inaongeza  kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wananchi waweze kunufaika", amesema Dkt.Mwigulu

Naibu Waziri wa Ujenzi  mhandisi .Godfrey Kasekenya amesema  katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali  imetenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini ikiwemo mkoa wa Mara  ambapo ujenzi wa barabara Makutano -Butiama km 50 utekelezaji wake umekamilika.

Amezitaja barabara za Makutano- Butiama -Nyamuswa-fort Ikoma hadi Ngorongoro gate  sehemu ya  Sanzate-Nata km 40 ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 67. 

Mhandisi Kasekenya amesema  Serikali imetoa kipaumbele pekee katika utekelezaji wa barabara za Wilaya ya Butiama kutokana  na historia ya Baba wa Taifa Mwl.Julias Nyerere Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naibu Waziri Kasekenya ameelekeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha inafunga taa kwenye barabara zote zenye lami katika miji na Wilaya mkoani Mara ili wananchi waweze kufanya shughuli zao usiku na mchana, kupendezesha miji na kuongeza  usalama.