TANROADS YAIMARISHA UKUSANYAJI WA TAARIFA ZA BARABARA KWA KUNUNUA MTAMBO WA KISASA
Morogoro, 03 Julai, 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeimarisha ukusanyaji wa taarifa za hali ya barabara za lami kwa kununua mtambo wa kisasa utakaoongeza usahihi wa tathmini za matengenezo, ukarabati na usalama wa barabara.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya matumizi ya mtambo huo mpya yanayofanyika mkoani Morogoro, Mhandisi wa Usimamizi wa Samani, Bw. Ndaji Mayige, amesema mafunzo hayo yanawashirikisha wataalamu kutoka ofisi za TANROADS za mikoa ya Pwani, Shinyanga, Dodoma, Iringa, Morogoro pamoja na Makao Makuu.
Amesema mtambo huo unarahisisha ukusanyaji, uchakataji na uchambuzi wa taarifa za hali ya barabara, hatua zinazowezesha kuandaa makadirio sahihi ya bajeti za matengenezo na ukarabati.
“Mtambo huu utatuwezesha kupata makadirio sahihi ya gharama za matengenezo. Hapo awali wakati mwingine tulikadiria bajeti ndogo kuliko uhalisia na hivyo kulazimika kuomba nyongeza ili kukamilisha kazi,” amesema Mhandisi Mayige.
Ameongeza kuwa huu ni mtambo wa pili wa aina hiyo kununuliwa na Serikali, baada ya wa kwanza kununuliwa mwaka 2022. Tofauti na mtambo wa awali, mtambo huu umeongezewa vifaa vinavyokusanya taarifa za kutathmini usalama wa barabara, hivyo kusaidia kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili kupunguza ajali.
Vilevile, amesema mtambo huo una uwezo wa kufanya sensa ya samani za barabarani kwa usahihi na kwa muda mfupi kupitia picha zenye ubora wa hali ya juu, hali inayowezesha wataalamu kufanya uchambuzi wakiwa ofisini na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miundombinu ya barabara.