News

WAZIRI MKUU AIAGIZA TANROADS KUTANGAZA ZABUNI YA UTEGI-SHIRATI KM 27

WAZIRI MKUU AIAGIZA TANROADS KUTANGAZA ZABUNI YA UTEGI-SHIRATI KM 27

 Rorya, 02 Julai, 2026

Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu  Lameck Nchemba ameielekeza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuanza ujenzi wa barabara ya Utegi-Shirati yenye urefu wa km 27 kwa kiwango cha lami.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo mjini Rorya  katika ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani Mara na kusisitiza kuwa baada ya Serikali kutekeleza maamuzi ya kimkakati kwa maslahi ya taifa sasa ni wakati wa kutekeleza miradi ya barabara za mikoa ukiwemo mkoa wa Mara pamoja na wilaya zake.

 “Nakuelekeza Meneja Mkoa wa Mara TANROADS mara baada ya kumalizika ziara hii tangaza zabuni kwa Wakandarasi na hakikisha Mkandarasi anapatikana ujenzi wa mradi huu uanze mara moja , “amesema Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Serikali imeelekeza fedha zote zinazokusanywa  kwenye mifuko ya barabara kwa ajili ya ujenzi wa barabara za TANROADS na TARURA kupelekwa kwenye miradi hiyo mara moja kwa ajili ya utekelezaji ili kuleta tija.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ameahidi na kumhakikishia Waziri Mkuu kutangaza zabuni kwa Wakandarasi ndani ya muda mfupi ili kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kuzingatia  thamani ya fedha.

Mhandisi Kasekenya amesema  Serikali  inajenga  barabara ya Rorya-Kirongwe yenye urefu wa kilomita 62 kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuhamasisha shughuli za kiuchumi, kijamii na huduma za usafiri na usafirishaji.

Ameeleza  kuwa Serikali imetoa kipaumbele cha kufanya ukarabati mkubwa wa shoroba zote za kiuchumi ikiwemo Barabara ya Mwanza hadi Lamadi na baada ya kukamilisha mradi wa barabara ya Utegi-Shirati Serikali itaendelea na utekelezaji kwa barabara zilizobaki ili kujenga kwa kiwango cha lami.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano uliofanyika wilayani Rorya mkoani Mara ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake Mkoani Mara.