News

SERIKALI YAPELEKA VICHEKO BARABARA YA MAKAMBAKO–SONGEA

SERIKALI YAPELEKA VICHEKO BARABARA YA MAKAMBAKO–SONGEA

Songea, 02 Julai, 2026

Serikali imeanza ujenzi mpya wa barabara inayounganisha mikoa ya Njombe na Ruvuma baada ile ya awali kuanza kuchoka kutokana na kutumika kwa zaidi ya miaka 40.

Akizungumza katika uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema barabara hiyo ni ya kimkakati kwa umuhimu wake kwa mikoa husika na taifa kwa ujumla.

“Mikoa ya Ruvuma na Njombe inazalisha chakula kingi kwa taifa na hivyo ni muhimu sana kwa mazao kusafiri kwa uhakika kutoka kwa wakulima kwenda yalipo masoko na pia biashara ya makaa ya mawe ambayo nayo inashamiri.

“Barabara ya Makambako–Songea si mali ya wananchi wa Songea au Ruvuma pekee, bali ni mradi wa kimkakati wenye manufaa kwa Watanzania wote kutokana na mchango wake katika kuimarisha uchumi na kurahisisha huduma za usafiri nchini,” amesema Ulega.

Aidha, Waziri huyo amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kuifanya Ruvuma kuwa kitovu cha biashara katika Ukanda wa Kusini na kufungua fursa zaidi za uwekezaji na maendeleo ya uchumi. 

Mradi wa barabara ya Makambako–Songea (km 295), sehemu ya Songea–Litukila (km 100) pamoja na barabara ya mchepuo ya Songea (km 16), unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Tanzania Transport Integration Project (TanTIP) kwa gharama ya Shilingi bilioni 158.7.

Mradi huo utahusisha pia ujenzi wa daraja moja kubwa, madaraja madogo 11, makalvati 2,436, usimikaji wa taa za barabarani 2,224 pamoja na ujenzi wa mzani mpya wa kisasa katika eneo la Luhimba, hatua zinazotarajiwa kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara, kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa na kuchochea ukuaji wa uchumi katika Ukanda wa Kusini.

Ulega alisema kwa kuanzia serikali itaanza na ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu ya Songea–Litukila yenye urefu wa kilometa 100 pamoja na barabara ya mchepuo ya Songea yenye urefu wa kilometa 16 na mkandarasi atakuwa ni kampuni ya Zhongan Hauli Construction Group.

Waziri huyo amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha kasi ya utekelezaji inaendana na matarajio ya wananchi, huku akisisitiza kuwa mradi huo ni wa kimkakati wenye umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.

Kwenye tukio hilo, Ulega alitoa maelekezo kwa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na mkandarasi kupanga utekelezaji wa kazi kwa ufanisi kwa kugawa maeneo ya ujenzi katika vipande vinavyotekelezeka badala ya kufungua sehemu ndefu za barabara ambazo hazikamilishwi kwa wakati, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi na watumiaji wa barabara.

"Ninawasihi na kuwataka TANROADS na mkandarasi msiweke vipande virefu virefu vya ujenzi, Utakuta barabara mkandarasi anaitifua kilometa 50 kati ya hizi 100, sasa unajiuliza kwanini atifue barabara hii kote huko", amesisitiza Ulega. 

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed amesema barabara ya Songea–Makambako ni miongoni mwa miradi ya kimkakati yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na jamii kwa mikoa ya Kusini, hususan Mkoa wa Ruvuma ambao ni kitovu cha uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula, yakiwemo mahindi, soya, maharage na kahawa.