News

WAZIRI MKUU ATAKA BARABARA MKOANI MARA ZIJENGWE KWA HARAKA

WAZIRI MKUU ATAKA BARABARA MKOANI MARA ZIJENGWE KWA HARAKA

Mara, 01 Julai, 2026

Waziri Mkuu  Dkt. Mwigulu Nchemba  ameitaka Wizara ya Ujenzi kuhakikisha barabara za lami zinazojengwa mkoani Mara kukamilika haraka.

Akizungumza mjini Mugumu katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara Dkt. Mwigulu amesema baada ya Serikali kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati sasa inaelekeza nguvu kwenye barabara hususan za mkoani Mara.

Dkt. Nchemba amezitaja barabara hizi kuwa ni barabara ya Sanzate-Nata (km 40), Tarime-Mugumu (km 25) na Nyamongo-Mugumu ambapo Wakandarasi wanatakiwa kuendelea na ujenzi, ili waweze kukamilisha kwa muda uliopangwa kuanzia sasa.

“Niwatoe hofu fedha zote za miradi zinazokusanywa na mfuko wa barabara zitakwenda moja kwa  moja kwenye  kukamilisha miundombinu ya barabara hizo“ amesisitiza Waziri Mkuu.

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema dhamira ya Serikali ni kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwa lami pamoja na Wilaya zake ikiwemo mkoa wa Mara ili kuchochea shughuli za kitalii, madini, uvuvi na ufugaji. 

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi hiyo katika mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo barabara ya Tarime Mjini-Mogabiri yenye urefu wa km 9.3 inaendelea kujengwa  na mkandarasi ameshasaini mkataba. 

Mradi mwingine ni barabara ya Mogabire-Nyamongo (km 25)  unajengwa na mkandarasi mzawa ambapo tayari ameshakamilisha kilometa 15 katika mradi huo na anaendelea kujenga sehemu iliyobaki.

Naibu Waziri Mhandisi Kasekenya amefafanua  kuwa  ujenzi wa barabara ya,Nyamongo-Mugumu unatekelezwa na kampuni Stakle pamoja na barabara za maingilio na baada ya kukamilika barabara hiyo itafungwa taa ili ziweze kupitika usiku na mchana.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu yupo katika ziara ya siku tano mkoani Mara yenye lengo la kukagua shughuli za maendeleo na kutatua changamoto  mbalimbali za wananchi.