News

SERIKALI YAONGEZA MITAMBO YA KUKAGUA UBORA WA BARABARA 

SERIKALI YAONGEZA MITAMBO YA KUKAGUA UBORA WA BARABARA 

Morogoro, 01 Julai, 2026

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imenunua mtambo wa kisasa wa Laser Cracks Measuring System (LCMS) kwa ajili ya kukagua ubora wa barabara za lami na kusaidia kupanga matengenezo kwa usahihi, pamoja na kuthibitisha ubora wa barabara mpya kabla ya kukabidhiwa Serikalini.

Akizungumza mjini Morogoro wakati wa mafunzo ya wataalamu yanayoendeshwa na wawezeshaji kutoka New Zealand, Meneja Usimamizi wa Samani za Barabara wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Leonard Mombia, amesema mtambo huo umefungwa kwenye gari na una vifaa vya kisasa ikiwemo kamera, kompyuta na sensa za laser zinazobaini hitilafu mbalimbali kama nyufa, mashimo, unyogovu wa magurudumu, kubadilika kwa lami na kutokomeka kwa mawe.

Amesema tofauti na ukaguzi wa awali uliotegemea kutembea kwa miguu na macho, LCMS hukagua barabara kwa kasi ya zaidi ya kilometa 100 kwa saa na kutoa vipimo sahihi vya urefu, upana na kina cha nyufa, hivyo kurahisisha upangaji wa matengenezo.

Mhandisi Mombia ameongeza kuwa mtambo huo pia hutumika kimataifa kukagua barabara za kurukia na kutua ndege, maeneo ya bandarini na kufanya tathmini za usalama wa barabara (iRAP), zinazosaidia kubaini barabara zinazohitaji matengenezo ya haraka ili kupunguza ajali.

Baada ya mafunzo ya nadharia, wataalamu watafanya mafunzo ya vitendo kwenye barabara za Mkoa wa Morogoro kabla ya kuchambua taarifa zitakazozalishwa na mtambo huo.

Ameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo, akieleza kuwa utaongeza ufanisi wa ukaguzi na uratibu wa matengenezo ya barabara. Kwa sasa, TANROADS inasimamia mitambo minne ya kisasa ya ukaguzi wa barabara kuu na za mikoa.