TANROADS YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA TUZO ZA EAST AFRICA PUBLIC SERVICE AWARDS 2026
Dar es salaam, 30 Juni,2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeibuka mshindi wa jumla wa Tuzo ya Umahiri wa Miundombinu ya Barabara Afrika (African Road Infrastructure Excellence Award 2026) katika hafla ya Tuzo za Utumishi wa Umma Afrika Mashariki (East Africa Public Service Awards 2026) iliyofanyika Juni 30, 2026 katika Hoteli ya Serena.
TANROADS imetwaa tuzo hiyo baada ya kuibuka kinara miongoni mwa washiriki katika makundi mbalimbali ya tuzo na kutangazwa kuwa mshindi wa jumla (Overall Winner) wa mashindano hayo yaliyolenga kutambua taasisi zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma za umma na maendeleo ya miundombinu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango mkubwa wa TANROADS katika maendeleo ya miundombinu ya barabara, kuimarisha uunganishaji wa maeneo mbalimbali kwa njia za usafiri (national connectivity), kuongeza ufanisi wa usafiri (transport efficiency), kuendeleza ubora wa uhandisi (engineering excellence) pamoja na kujenga na kusimamia mtandao endelevu wa barabara (sustainable road networks) nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Tuzo hiyo imepokelewa kwa niaba ya TANROADS na Kaimu Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa Wakala huo, Aisha Malima, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma.
Ushindi huo unaendelea kuthibitisha nafasi ya TANROADS kama taasisi inayoongoza katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara yenye viwango vya kimataifa, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi, kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo, pamoja na kuimarisha mtandao wa usafiri ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki.