News

MIRADI YA TANROADS DODOMA KUCHOCHEA MAENDELEO NA KUBORESHA MAISHA YA WANANCHI – MTENDAJI MKUU

MIRADI YA TANROADS DODOMA KUCHOCHEA MAENDELEO NA KUBORESHA MAISHA YA WANANCHI – MTENDAJI MKUU

Dodoma, 23 Juni, 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika Jiji la Dodoma inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, kuchochea ukuaji wa uchumi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, alipotembelea banda la taasisi hiyo katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofikia kilele tarehe 23 Juni 2026 katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Mhandisi Besta amesema miradi inayotekelezwa na TANROADS ikiwemo barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma, Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato pamoja na mradi wa barabara ya njia sita kutoka katikati ya jiji kuelekea Chamwino, itaongeza fursa za kiuchumi, kupunguza muda wa safari na kuboresha huduma kwa wananchi.

Ameeleza kuwa barabara ya mzunguko wa nje iliyofikia takribani asilimia 95 ya utekelezaji itasaidia kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji, wakati Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kitafungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na utalii.

Aidha, mradi wa barabara ya njia sita utarahisisha usafiri wa wananchi na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi katika mji mkuu wa nchi.

“Miradi hii inalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za usafiri na usafirishaji zilizo bora, salama na zenye kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema Mhandisi Besta.

Ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo, TANROADS imetoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama barabarani, uhifadhi wa barabara, utunzaji wa mazingira na umuhimu wa kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti baada ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

Maadhimisho hayo yamefungwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe.