News

ULEGA:MIKOPO NAFUU IMEFUNGUA TANZANIA KWA MIUNDOBINU YA KISASA

ULEGA:MIKOPO NAFUU IMEFUNGUA TANZANIA KWA MIUNDOBINU YA KISASA

Dodoma, 22 Juni, 2026

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Serikali imekuwa ikikopa mikopo nafuu kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya kisasa ya barabara na viwanja vya ndege nchini, akisisitiza kuwa mikopo hiyo imeleta matokeo makubwa yanayoonekana kwa wananchi.

Akichangia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 bungeni leo, Ulega alipinga kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa upinzani kwamba Serikali inaendelea kukopa bila kutekeleza miradi ya maendeleo, akizitaja kauli hizo kuwa za uzushi na zinazolenga kuwachonganisha wananchi na Serikali.

“Nataka niwaambie kwamba hakuna fedha zilizokopwa ambazo zimeshindwa kuleta maendeleo. Katika sekta ya barabara na viwanja vya ndege vinavyosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, ushahidi wa matumizi ya mikopo hiyo unaonekana wazi,” alisema Ulega.

Alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuimarisha miundombinu nchini, akieleza kuwa mikopo nafuu imewezesha ukarabati na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Tabora, Shinyanga, Sumbawanga, Kigoma, Tanga na Manyara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

Ulega alisema mafanikio hayo yanaonekana pia katika sekta ya usafiri wa anga, ambapo hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi amekuwa akizindua na kufungua viwanja mbalimbali vya ndege pamoja na kuruhusu safari za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hatua inayolenga kuchochea uchumi na kurahisisha usafiri wa wananchi.

Aidha, alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, ambao unatarajiwa kuwa kitovu kikubwa cha usafiri wa anga nchini na ukanda wa Afrika Mashariki kwa kupokea ndege kutoka mataifa mbalimbali.

Katika upande wa barabara, Ulega alisema mikopo hiyo imewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya njia sita kutoka Ikulu ya Chamwino hadi Jiji la Dodoma, pamoja na maendeleo ya mji wa kisasa wa Serikali katika makao makuu ya nchi.

Kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, Waziri huyo alisema mikopo nafuu imechangia kukamilika kwa miradi muhimu ya barabara ikiwemo Malagarasi–Uvinza na Kasulu–Manyovu, ambayo imeimarisha usafiri na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Aliongeza kuwa wananchi wa mikoa ya kusini wameondokana na changamoto ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara kutokana na ujenzi wa Daraja la Somanga–Mtama pamoja na madaraja mengine 81 yaliyojengwa kupitia Mradi wa Dharura wa Ujenzi wa Madaraja (CERC).

“Leo kupitia mikopo hii nafuu na maono ya Rais Samia, wananchi wengi wamepata huduma bora za usafiri na mawasiliano. Haya ni maendeleo yanayoonekana na kugusa maisha ya Watanzania moja kwa moja,” alisema Ulega.