News

WANANCHI WAKOSHWA NA MAELEZO MAZURI KWENYE BANDA LA MAONESHO LA TANROADS

WANANCHI WAKOSHWA NA MAELEZO MAZURI KWENYE BANDA LA MAONESHO LA TANROADS

Dodoma, 19 Juni, 2026

Wananchi na wakazi wa jiji la Dodoma na kutoka mikoa ya jirani wameridhishwa na maelezo mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa na wataalam kwenye banda la maonesho la Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kwenye viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea banda hilo, Bw. Abdulrahman Nyerembe amesema amejifunza tofauti ya TANROADS na TARURA, ambapo awali taasisi hizi zilikuwa zikimchanganya.

Pia ameridhishwa na maelezo kuwa TANROADS hawatengenezi barabara tu, pia walikasimiwa ujenzi wa viwanja vya ndege, ambapo sasa wapo katika hatua za ukamilishaji wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato.

Amesema anaona fahari na kujivunia mafanikio TAROADS katika ujenzi wa miundombinu madhubuti.

Aidha, ametoa wito kwa watumiaji wa barabara kuhakikisha wanazilinda na kuzitunza na wasiziharibu, ili ziweze kudumu na kutumiwa na kizazi hata kizazi, ambapo serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi za ndani na hata za wadau wa maendeleo kwa ajili ya ujenzi.

Naye, Bi. Amina Juma amesema amenufaika kwa kujifunza mengi ikiwemo ujengaji wa barabara kuu na za mikoa, ambazo zinaunganisha mikoa mbalimbali pamoja na nchi jirani.

Bi. Amina amesema pia TANROADS wamekuwa vinara wa kutunza mazingira katika kila mradi ambapo wamekuwa wakirudisha hali ya uhalisia wa eneo kama ilivyokuwa kabla ya ujenzi.

Hatahivyo, Bi. Amina amewaita wananchi kuja kupata elimu kwenye banda la TANROADS, ambazo zitawasaidia katika shughuli mbalimbali.Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yalianza tarehe 16 Juni na yanatarajia kumalizika Juni 23, ambapo kaulimbiu inasema: “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”.