MKURUGENZI WA UTAWALA TIRA AIPONGEZA TANROADS KWA KUPUNGUZA FOLENI ZA MAGARI
Dodoma, 17 Juni 2026
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Bw. Nakaunda Baraka, ameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuendelea kujenga miundombinu ya kisasa ya barabara inayochangia kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri katika maeneo mbalimbali nchini.
Bw. Nakaunda ametoa pongezi hizo leo, Juni 17, 2026, alipotembelea banda la TANROADS katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, amesema Barabara ya Mzunguko wa Nje wa Jiji la Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) imeanza kuleta matokeo chanya kwa kupunguza foleni iliyokuwa ikisababishwa na magari makubwa, hususan ya mizigo, yaliyokuwa yakipita katikati ya jiji. Amesema kwa sasa magari hayo yanaingia kupitia eneo la Sheli ya Jeshi Mtumba na kuunganika na barabara katika eneo la Nala bila kulazimika kupita katikati ya mji.
Aidha, amesema mradi wa ujenzi wa daraja la juu la magari (flyover) unaotarajiwa kutekelezwa eneo la Mtumba utaongeza ufanisi wa usafiri na kusaidia zaidi kupunguza msongamano wa magari kadri Jiji la Dodoma linavyoendelea kukua.
"Ninaipongeza sana TANROADS kwa kazi kubwa inayoifanya. Kwa sasa foleni imepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu magari mengi ya mizigo hayapitii tena katikati ya jiji. Hii imeongeza urahisi wa usafiri kwa wananchi na kupunguza muda wa safari," amesema Bw. Nakaunda.
Pia amewataka wananchi kutunza miundombinu ya barabara kwa kuepuka vitendo vya uharibifu na kujiepusha na ujenzi ndani ya hifadhi za barabara, akibainisha kuwa vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara na kusababisha hasara za mali.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo "Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu", yakilenga kuwakutanisha wananchi na taasisi mbalimbali za umma ili kupata elimu, huduma na taarifa kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Serikali kwa maendeleo ya Taifa.