News

UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI KUTATUA KERO YA MAFURIKO, MRADI WAFIKIA ASILIMIA 34

UJENZI WA DARAJA LA JANGWANI KUTATUA KERO YA MAFURIKO, MRADI WAFIKIA ASILIMIA 34

Dar es Salaam, 14 Juni, 2026

Serikali inaendelea na ujenzi wa Daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam, mradi unaolenga kutatua tatizo la muda mrefu la mafuriko ambalo limekuwa likisababisha usumbufu wa usafiri, kuhatarisha maisha ya wananchi na kuathiri shughuli za kiuchumi. 

Hadi sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 34, ambapo Meneja wa mradi, Mhandisi Leonard Ngayungi, kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), amesema daraja hilo linajengwa chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Bonde la Mto Msimbazi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya Shilingi bilioni 97.1 na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24.

Amesema hatua muhimu zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa daraja la muda linalotumika kwa sasa, ambapo hata katika msimu wa mvua uliopita hakukuwa na magari yaliyokwama kutokana na mafuriko.

Aidha, Mhandisi Ngayungi amesema nguzo 432 kati ya 496 za msingi wa daraja tayari zimekamilika, pamoja na nguzo kuu 24 kati ya 48 zinazobeba daraja.

Mhandisi Ngayungi ameeleza kuwa mradi ukikamilika utaondoa changamoto ya mafuriko katika eneo la Jangwani, kurahisisha usafiri na usafirishaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara na kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Mbali na manufaa ya miundombinu, mradi huo pia umechangia ajira kwa wananchi, ambapo hadi sasa watu 232 wamepata ajira za moja kwa moja katika utekelezaji wake.

 Serikali imeendelea kutoa fedha kwa wakati, hali inayowezesha kazi kuendelea vizuri kulingana na ratiba iliyopangwa.