MAABARA ZA TANROADS ZAHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA MIUNDOMBINU BORA NA SALAMA
Dodoma, 12 Juni 2026
Uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) katika kuimarisha maabara za upimaji wa malighafi unalenga kuhakikisha wananchi wanapata barabara na miundombinu mingine ya usafiri yenye ubora, usalama na uwezo wa kudumu kwa muda mrefu.
Maabara za TANROADS zinafanya kazi muhimu ya kupima malighafi mbalimbali zinazotumika katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo maji, udongo, mchanga, kokoto, lami na nondo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Hatua hii husaidia kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa inakidhi ubora unaotakiwa kabla ya kuanza kutumiwa na wananchi.
Mhandisi Getrude Enock wa Idara ya Maabara TANROADS Mkoa wa Dodoma amesema kuwa maabara hizo zimeboreshwa kwa vifaa vya kisasa vinavyowezesha kufanya vipimo vya uhakika na kutoa matokeo yanayoendana na viwango vya kimataifa.
“Tunafanya vipimo kuanzia hatua ya usanifu wa mradi hadi baada ya ujenzi kukamilika. Hii inatusaidia kuhakikisha kuwa miundombinu inayokabidhiwa kwa wananchi inakidhi viwango vya ubora vilivyopangwa tangu mwanzo,” amesema Mhandisi Getrude.
Ameeleza kuwa uwepo wa maabara hizo unasaidia kuzuia matumizi ya malighafi zisizo na ubora ambazo zinaweza kusababisha miundombinu kuharibika mapema na kuongeza gharama za matengenezo.
Matokeo yake ni wananchi kupata huduma bora za usafiri, usalama zaidi wanapotumia barabara pamoja na matumizi sahihi ya fedha za umma.Kwa mujibu wa Mhandisi Getrude, maabara za TANROADS pia zinatoa huduma za upimaji kwa wadau wengine wa sekta ya ujenzi ili kuhakikisha miradi mbalimbali nchini inajengwa kwa viwango vinavyokubalika.Amehimiza wajenzi na wadau wa sekta ya ujenzi kutumia huduma za maabara za TANROADS ili kuhakikisha malighafi wanazotumia zinakidhi viwango vya ubora vinavyohitajika, jambo litakalochangia ujenzi wa miundombinu imara na yenye manufaa kwa jamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.