News

MAAFISA RASILIMALI WATU NA UTAWALA TANROADS WAJENGEWA UWEZO WA MFUMO WA E-LIKIZO 

MAAFISA RASILIMALI WATU NA UTAWALA TANROADS WAJENGEWA UWEZO WA MFUMO WA E-LIKIZO 

Dar es Salaam, 11 Juni, 2026

Maafisa Rasilimali watu na Utawala, na  wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kutoka mikoa mbalimbali wameshiriki kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa shughuli za idara pamoja na kunolewa kuhusu mfumo wa kieletroniki wa usimamizi wa likizo (e-leave).

 Mafunzo hayo yalifunguliwa na Kaimu Mkurugenzi Wa Huduma za Uendeshaji Bw. Elirehema Saiteru, ambaye amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo maafisa hao katika matumizi sahihi ya mfumo huo wa Serikali.

Bw. Saiteru amesema kuwa  mafunzo hayo yatakayotolewa na Mkufunzi kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, yatawaongezea weledi washiriki, ambapo kwa muda mrefu TANROADS imekuwa ikitumia mifumo mbalimbali katika kusimamia taarifa za watumishi.

“Mafunzo haya ni maelekezo ya Serikali ya kutumia Mifumo Jumuishi katika kutoa huduma za Serikali, na usimamizi wa Rasilimali watu ikiwemo Mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi wa likizo (e-leave),” amesema Bw. Saiteru.

Hivyo, basi kupitia mafunzo haya, Maafisa Tawala na Rasilimali watu watapata ujuzi wa kuingiza na kuhakiki taarifa za watumishi zinazohusiana na masuala ya likizo pamoja na kumbukumbu nyingine za watumishi katika taasisi.

Aidha, pamoja na mafunzo hayo kikao hicho kitajadili pia tathmini ya utekelezaji wa shughuli zilizopangwa tangu mwanzo wa mwaka hadi sasa,kwa lengo la kubaini mafanikio yaliyopatikana,changamoto zilizojitokeza na maeneo yanayohitaji maboresho ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Halikadhalika, kikao kazi hicho kinatarajiwa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wataalamu wa rasilimali watu na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya taasisi.