News

KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA CHA MSALATO KUANZA KUTUMIKA SEPTEMBA 2026 

KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA CHA MSALATO KUANZA KUTUMIKA SEPTEMBA 2026 

Dodoma, 10 Juni, 2026

Serikali imesema Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa wa Msalato unaojengwa jijini Dodoma unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika mwezi Septemba 2026, hatua itakayoongeza uwezo wa usafiri wa anga na kuimarisha nafasi ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo Juni 10, 2026, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

“Kila kitu kikifika kwa wakati, ndani ya mwezi Septemba mwaka huu uwanja wetu utakuwa umekamilika na uko tayari kwa matumizi,” amesema. Waziri huyo.

Amesema Kiwanja huo wa kisasa utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria Milioni 1.5 kwa mwaka na kupokea ndege kubwa za ndani na kimataifa, jambo litakalorahisisha usafiri, kukuza biashara, utalii na kuvutia uwekezaji zaidi Dodoma.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kiwanja huo ni mradi wa kimkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na umesanifiwa kwa viwango vya kisasa pamoja na uwezo wa kupanuliwa kadri mahitaji yatakavyoongezeka.

Naye Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Japherson Nnko, amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 86.73 huku ajira 2,117 zikiwa zimezalishwa tangu kuanza kwa ujenzi wake.

Kukamilika kwa uwanja huo kunatarajiwa kuifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha usafiri wa anga nchini na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.